Aliyekua kiungo wa mabingwa wa soka nchini England Manchester City Yaya Toure, huenda akaihama klabu ya Olympiakos Ugiriki, kufuatia kushindwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

Toure alijiungana klabu hiyo ambayo aliwahi kuitumikia kuanzia mwaka 2005–2006, miezi mitatu iliyopita kama mchezaji huru, baada ya kuachwa na Man City kufuatia pendekezo la meneja Pep Guardiola.

Wakala wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35 Dmitri Seluk, amezungumza na gazeti la michezo la Italia (Gazzetta Della Sports) na kueleza dhamira yake ya kutaka kuvunja mkataba wa mtaja wake, endapo ataendelea kusota benchi.

Seluk amesema suala la kukaa benchi kwa mchezaji wake haikua makubaliano na uongozi wa Olympiakos, na hafahamu nini kinachomsibu Toure hadi kufikia hali hiyo, wakati bado ana uwezo wa kucheza soka.

“Hatuhitaji kuwaumiza mashabiki wa Olympiakos. Nimeshawaarifu viongozi wao kuhusu jambo hili, na kama tutavunja mkataba hatutadai chochote kama fidia, maana wao ndio sababu kama haya yatatokea,”

“Makubaliano yalikua Toure acheze kwenye kikosi cha kwanza, na yapo kwenye mkataba, sasa kwa dhamira njema nimewaarifu na ninatarajia kuona mabadiliko, kama itakua tofauti sitosita kufanya nilichokwambia.” Alisema Seluk.

“Toure ana uwezo mkubwa kisoka na ana kila sababu ya kuisaidia Olympiakos kufikia lengo lake msimu huu, ndio maana tulikubali arudi Ugiriki, alikataa klabu kadhaa, tena kubwa ambazo zingempa nafasi ya kucheza kama ilivyokua Man city.”

“Kama itashindikana kuna klabu nyingi zinahitaji huduma yake hususan Saudi Arabia, Japan na China. Tutakapovunja mkataba hatuna budi kuzikubalia ili maisha ya mchezaji wangu ya kucheza soka yaendelee.”

Video: BoT yabaini ongezeko la biashara ya ubadilishaji fedha kinyume cha utaratibu
Video: Tume ya Taifa ya Umwagiliaji yatakiwa kuhakiki eneo linalofaa kwa kilimo