Wakala wa kiungo kutoka Ivory Coast Yaya Toure, amethibitisha mchezaji wake kufanyiwa vipimo vya afya jijini London, tayari kwa usajili ndani ya klabu yenye maskani yake makuu jijini humo ambayo hakua tayari kuitaja.

Toure amekua katika mchakato wa kusaka klabu ya kuitumikia msimu huu, baada ya kuachwa na Man City mwishoni mwa msimu uliopita, huku akiacha kumbukumbu ya kuitumikia klabu hiyo ya Etihad Stadium kwa muda wa miaka minane.

Klabu kadhaa za England zilionyesha nia ya kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35, lakini wakala wake Dimitry Seluk alikua kimya katika kipindi chote cha dirisha la usajili, ambapo kwa England lilifungwa rasmi kati kati ya mwezi huu.

“Yaya amepita katika vipimo vya afya jijini London, Yaya anakaribia kusaini mkataba mpya.” Aliandika Dimitry Seluk kwenye ukurasa wake wa tweeter.

Klabu ya West Ham Utd yenye maskani yake jijini London, imekua ikitajwa kuwa mstari wa mbele kutaka kumsajili kiungo huyo, huku uwepo wa meneja Manuel Pellegrini ambaye aliwahi kufanya kazi na Toure wakiwa Man City ukihusishwa, na mipango wa mchezaji huyo kuhamia London Stadium.

Hata hivyo Seluk amethibitisha kuwa London Stadium, sio mahala ambapo mchezaji wake atakapocheza soka kwa msimu huu, na badala yake amewataka mashabiki wa soka duniani kuendelea kusubiri.

“Ninahakikisha kwa asilimi 100 sio West Ham,” “Yaya ni mchezaji mwenye sifa ya kuwa bingwa.”

Toure aliondoka Man City huku akiwa amecheza michezo 316 na kufunga mabao 79. Alitwaa ubingwa wa England mara tatu akiwa na klabu hiyo ya mjini Manchester, Kombe la FA Cup na Kombe la ligi mara mbili.

Real Madrid yawashiwa taa ya kijani usajili wa Mariano
Kocha wa Stars Awatema wachezaji wa Simba