Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Fredrick Mwakalebela amesema uongozi wa timu hiyo utamchukulia hatua winga Bernard Morrison kufuatia kitendo chake cha kukacha kukaa kwenye benchi baada ya kufanyiwa mabadiliko katika mchezo wa nusu fainali kombe la Shirikisho dhidi ya Simba SC.

Katika mchezo huo ambao Young Africans ilikubali kipigo cha mabao manne kwa moja, baada ya kufanyiwa ‘sub’, Morrison ‘alimvimbia’ mwamuzi pale alipojaribu kumzuia asiondoke eneo la uwanja na hata kumsukuma na kuelekea katika vyumba vya kubadilishia nguo na kisha kuondoka moja kwa moja kwa usafiri wa Bodaboda.

Mwakalebela amesema Morrison ataitwa mbele ya Kamati inayohusika na masuala ya Nidhamu ndani ya klabu ya Young Africans na atachukuliwa hatua kulingana na makosa yake.

“Hakuna aliyefurahishwa na tukio lililofanywa na mchezaji wetu Bernard Morrison kwenye mchezo dhidi ya watani zetu Simba. Akiwa mchezaji wa Yanga mwenye mkataba halali, tutakaa nae na kumsikiliza kisha ataadhibiwa kulingana na makosa aliyofanya,” alisema Mwakalebela.

Kumekuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Young Africans ambao wengi wameonyesha kutomuhitaji tena mchezaji huyo katika timu yao.

Mwanachama na Mhamasishaji maarufu Jimmy Msindo ‘Kindoki’, amesema yeye kama shabiki kindakindaki wa Young Africans hatakuwa tayari kuingia uwanjani kuishabikia timu yake kila itakapotokea jina la Morrison kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoshuka uwanjani.

Kindoki amemtaka Mghana huyo kujitokeza hadharani kuwaomba radhi mashabiki wa Young Africans kwa matukio yake ya utovu wa Nidhamu na aahidi hatayarudia tena, wanaweza kumsamehe.

Wiki iliyopita, Morrison aliingia katika mvutano na uongozi wa Young Africans akikana kuongeza mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo madai yake yaligonga mwamba TFF.

Alijiunga na Young Africans usajili wa dirisha dogo mwezi Januari akisaini mkataba wa miezi sita ambao unamalizika leo Julai 14.

Baada ya kuridhishwa na uwezo wake, uongozi wa Young Africans kupitia wadhamini wao GSM, walimuongeza mkataba wa miaka miwili akilipwa zaidi ya Tsh Milioni 70.

Nyota huyo ‘alivurugwa’ baada ya kupata ofa kutoka klabu moja huko Arabuni iliyokuwa imemuahidi kumlipa mshahara wa zaidi ya Dola 15,000 kwa mwezi.

Hai: Watuhumiwa dawa za kulevya, gongo watoroka mahabusu
Aristica Cioaba atangaza vita nafasi ya pili Ligi Kuu