Idara ya Habari na Mawasiliano ya Young Africans imethibitisha taarifa za kikosi chao kutarajiwa kuondoka nchini siku ya Ijumaa kuelekea Nigeria, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Brani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United.

Young Africans ilipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa kufungwa bao 1-0, Jumapili (Septamba 12) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Bumbuli amesema mipango na taratibu za safari ya kikosi chao inakwenda vizuri, na uongozi wa klabu hiyo hiyo umekodi ndege ya shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania).

Amesema msafara wa kuelekea nchini Nigeria utaambatana na mashabiki 48, ambao wanatarajiwa kuongeza hamasa kwa wachezaji, ambao watapewa nafasi ya kupambana kwenye mchezo wa mkondo wa pili, utakaochezwa Jumapili (Septamba 19) katika Uwanja wa Yakubu Gowon mjini Port Harcourt.

“Tutaondoka Ijumaa na ndege ya kukodi, tumetoa nafasi kwa mashabiki 48 ambao watakuwa kwenye msafara wa timu, na kwamba wanachotakiwa ni kuchangia dola 1,200 (Sh milion 2 kama gharama ya kwenda na kurudi, VISA na vipimo vya Uviko-19”) amesema Hassan Bumbuli.

Katika mchezo huo wa Jumapili (Septemba 19) Young Africans itatakiwa kusaka ushindi wa mabao 2-0 ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2021/22.

Wambura aipongeza Simba SC
Kesi ya Mbowe kuunguruma leo