Mashujaa wa Taifa, Young Africans wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho mchana wakitokea Angola, ambako jana walikata tiketi ya kuingia hatua makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Young Africans jana ilifungwa bao 1-0 na wenyeji Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania hatua hiyo Uwanja wa Esperanca mjini Dundo, Angola.

Lakini Young Africans wanakwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony.

Matokeo hayo si tu yanamaanisha Young Africans inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia yake, bali pia inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo ya michuano hivyo.

Awali ya hapo, Young Africans imewahi kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ikafuatiwa na mahasimu, Simba SC mwaka 2003.

Katika mchezo wa jana uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza, aliyesaidiwa na Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa wamekwishajipatia bao lao hilo.

Bao hilo lilifungwa na mkongwe Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama ‘Love Kabungula’ dakika ya 25, baada ya mabeki wa Young Africans kufanya uzembe kidogo.

Young Africans walitulia baada ya bao hilo, licha ya marefa kuonekana kabisa kupendelea wenyeji na wakafanikiwa kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nyuma kwa bao hilo moja tu.

Kipindi cha pili, Young Africans waliachana na mchezo wa kujihamia na kufunguka kuanza kushambulia, hali ambayo ilipunguza kasi ya wapinzani wao.

Kocha Mholanzi alimtoa kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko baada ya kuumia na kumuingiza Deus Kaseke dakika ya 69 aliyemalizia vizuri.

Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 72.

Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90 na ushei baada ya kumuangusha kwenye boksi mchezaji wa Esperanca na wenyeji wakapewa penalti, ambayo hata hivyo kipa Dida aliicheza.

Baada ya kuwasili, wachezaji wa Young Africans watakwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji mjini Songea Jumamosi na fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la ASFC Jumatano ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikumbukwe, Young Africans iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.

Young Africans ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Kikosi cha Young Africans kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva/Geoffrey Mwashiuya dk90, Thabani Kamusoko/Deus Kaseke dk69, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Kevin Yondan dk89 na Haruna Niyonzima.

Jogoo Wa Jiji Akubali Kuchinjwa Mjini Basel, Uswiz
Magari ya Washawasha yahamishiwa Zima Moto