Uongozi wa klabu ya Young Africans bado unaendelea kuwaaminisha Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuhusu usajili wa kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia, Clatous Chama, ambaye aliwahi kutamba akiwa na Simba SC kwa misimu mitatu mfululizo.

Young Africans wameibuka na taarifa za kuwa mbioni kumrejesha Kiungo huyo nchini Tanzania, tangu juma lililopita wakijinasibu watafanya hivyo ili kukiongezea nguvu kikosi chao, ambacho kwa msimu huu kimedhamiriwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

Hata hivyo sio mara ya kwanza kwa Young Africans kuhusishwa na mpango wa kumsajili Chama, kwani wamewahi kuingizwa kwenye mchakato huo katika misimu miwili ya usajili iliyopoita.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Young Africans, Eng. Hersi Said, amesema: “Chama ni moja kati ya viungo bora kuwahi kucheza katika ligi yetu, tungetamani kuwa naye wakati wowote ule na kwa sasa hakuna kinachoweza kuizuia Young Africans kufanya naye mazungumzo.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Young Africans, Dominic Albinus ‘Baba Paroko’ amesema: “Kwa sasa siwezi nikakanusha wala kukubali kuhusiana na hilo kwa kuwa ni mapema sana kulizungumzia, lakini kama kamati ya ufundi tunafanya kazi kwa karibu na benchi la ufundi, kama kutakuwa na taarifa rasmi basi tutaiweka wazi.”

Chama aliondoka Simba SC wakati wa usajili wa 2021/22 na kutimkia kwenye klabu ya RS Berkane inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco na kusaini mkataba wa miaka mitatu ambao utafikia kikomo Juni 30, 2024.

Polisi wakamata bastola 'ya Marekani'
Kansela Angela Merkel anena na vijana