Makamu wa Rais wa Young Africans Arafat Haji, ametamba kuwa hakuna wa kuwazuia kuteteta Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, baada ya kujizolea ushindi wa 3-1 dhidi ya Geita Gold FC.

Young Africans ilivuna ushindi huo nyumbani jijini Dar es salaam jana Jumapili (Machi 12), ikicheza katika Uwanja wa Azam Complex-Chamazi, huku ikitanguliwa kufungwa bao lililodumu ndani ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

Arafat amesema kila wakitazama michezo ya wapinzao wao walio ndani ya tano bora hawaoni timu itakayowazuia kuchukua taji la msimu huu, hivyo kinachofanyika kwa sasa ni kukamilisha ratiba na kusubiri kukabidhiwa taji lao kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.

Kiongozi huyo akaenda mbali zaidi akisema kinachoendelea sasa ni kuwa timu inashindana na malengo ya kikosi walichonacho kuwa katika ubora tofauti na timu zingine kiasi cha kuwaacha mbali wapinzani wao, Simba SC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 baada ya mechi 24.

“Tunalichukua tena hili taji, hili halina ubishi. kilichobaki sasa ni ukamil ishaji tu lakini kiushindani. Young Africans tuko katika eneo tofauti na wenzetu kiubora na ndio maana tumewaacha mbali,” amesema Arafat ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Zanzibar.

Amesema, kitu kikubwa ni ubora wa wachezaji wao wanaounda kikosi chao kuwa katika ubora mkubwa, pia kuwa na utulivu katika benchi lao la ufundi huku uongozi nao ukikamilisha kwa kiwango bora mahitaji ya timu yao.

“Angalieni kikosi chetu kilivyo katika ubora. wachezaji wenyewe tu wamekuwa katika ubora mkubwa lakini matunzo yao kwa maana ya mazoezi ya kiufundi yamekuwa yakiwaongezea thamani ukimtazama kocha wetu mkuu Nasreddine Nabi.”

“Huwa tunatazama ubora wa watu tunaoshindana nao, lakini sote tutakubaliana kuna umbali ambao tumewaacha wenzetu kiubora, Young Africans ubora wake uwanjani unajieleza na tutachukua taji hili mapema tu.

“Lakini juu yao upo uongozi ambao nao unakamilisha mahitaji yote muhimu yanayotoa utulivu wa idara zote kufanya kazi zao kwa mujibu wa inavyotakiwa hii ndio Young Africans ambayo tunataka iendelee kupiga hatua kubwa kama hizi.”

Denis Nkane asubiri ruhusa ya Nabi
Adel Amrouche atangaza jeshi la kuivaa Uganda