Kikosi kamili cha Yanga SC kinaondoka leo Dar es Salaam kwenda kisiwani Pemba kuweka kambi ya siku tano kujiandaa na mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Yanga watakuwa wenyeji wa Ahly, wapinzani wao wa kihistoria kwenye michuano ya Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 19 mjini Cairo, Misri.

Na baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba jana Uwanja wa Taifa, Yanga inayofundishwa na babu wa Kiholanzi, Hans van der Pluijm inalekea kambini Pemba leo kwa maandalizi ya mchezo mgumu ujao.

Wachezaji wote wa Yanga akiwemo Haruna Niyonzima ambaye anasumbuliwa na Malaria na pia hatacheza mechi ya kwanza dhidi ya Al Ahly kutokana na kuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano wanasafiri kwa ndege leo.

Kikosi cha Yanga kinachotarajiwa kuingia kambini leo ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.

Mabeki ni Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato Ngonyani, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Viungo ni Salum Telela, Mbuyu Twite (DRC), Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Issoufou Boubacar (Niger).

Washambuliaji ni Paul Nonga, Matheo Anthony, Malimi Busungu, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).

Benchi la Ufundi ni Kocha Mkuu, Hans van der Pluijm (Uholanzi), Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali

Daktari, Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa, Mohammed Mpogolo na meneja Hafidh Saleh.

Azam FC Waichunguza Esperance Hatua Kwa Hatua
Kamati Ya Nidhamu Ya TFF Yazishusha Timu Nne Za Ligi Daraja La Kwanza