Klabu ya Young Africans SC imetoa taarifa rasmi za kuachana na kiungo kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima, ambaye katika kipindi hiki amekua gumzo, baada ya dirisha la usajili wa Tanzania bara kufunguliwa Juni 15.

Niyonzima anadaiwa kuwa na mpango wa kusajiliwa na klabu ya Simba SC, hali ambayo ilizua taharuki kwa viongozi na mashabiki wa Young Africans SC, huku ikielezwa kwamba kiungo huyo bado ana mkataba na klabu hiyo ya Jangwani.

Katibu Mkuu wa Young Africans SC Boniface Mkwasa amesema Haruna Niyonzima amekua mchezaji wao kwa misimu sita tangu alipowasili nchini akitokea Rwanda alipokua akiitumikia APR, na wamejitahidi kufanya nae mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, lakini imeshindikana.

“Haruna Niyonzima bado ana mkataba mpaka mwezi Julai na Yanga SC, lakini hatutaweza kuendelea kuwa nae kwa msimu ujao kwani hatukuweza kufikia muafaka katika mazungumzo yetu na yeye licha ya timu yetu kuwa na nia za kuendelea nae kwa misimu miwili ijayo.

“Klabu inamtakia kila la kheri katika maisha yake na soka kwa ujumla.” Amesema Mkwasa.

Taarifa hizo zinatoa nafasi nzuri kwa Simba SC kuendelea na mpango wa kumsajili Haruna Niyonzima kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Chuji Wa Polisi Morogoro Ajisogeza Mtibwa Sugar
Usajili Wa Mohamed Salah Kuinufaisha Chelsea