Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara , Young Africans,  wamepiga hodi Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), wakitaka kupanguliwa ratiba ya ligi ili wapate muda mzuri wa kujiandaa kuikabili Simba.

Katika barua yao kwenda Bodi ya Ligi, Yanga inataka kupanguliwa ratiba ya mchezo wao dhidi ya Stand United uliopangwa kuchezwa Jumapili, Septemba 25.

Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Baraka Deusdedit, alisema jana wameomba mechi hiyo ichezwe Jumatano, Septemba 21, badala ya Jumapili, Septemba 25 kama ratiba ilivyoonyesha kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Deusdedit alisema kuwa wameomba mabadiliko hayo ili wapate nafasi ya kurejea Dar es Salaam Alhamisi kuanza rasmi mazoezi ya mapema kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Simba.

“Kama mchezo wetu utasogezwa nyuma na kuchezwa Jumatano, ina maana Alhamisi tungerejea Dar es Salaam na kujiandaa kwenda kuweka kambi Pemba kabla ya kupambana na Simba,” alisema Deusdedit.

Hata hivyo, Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas, alikaririwa akisema kua  hakuna barua yoyote kutoka Yanga iliyopokelewa na Bodi ya Ligi.

“Nimewasiliana na viongozi wa Bodi ya Ligi, wamenieleza hawajapokea barua yoyote kutoka Yanga kuomba mabadiliko ya ratiba ya mechi,” alisema Lucas.

Alisema hata kama maombi ya Yanga yatafika mezani kwao, hakuna uwezekano wa kupangua ratiba.

“Naomba niweke wazi, Young Africans, na Stand United watacheza mechi yao kwa tarehe ileile inayoonekana kwenye ratiba,” aliongezea kusema Lucas.

Yanga itakwenda kuweka kambi Pemba kwa siku sita kabla ya kurejea Dar es Salaam kuivaa Simba.

Kwa upande wa Simba, habari kutoka ndani zimedai kuwa uongozi umewataka wachezaji wake kucheza kwa tahadhari kubwa na kuepuka kuwa mejeruhi kwenye mechi dhidi ya Majimaji ili wawepo kwenye mchezo dhidi ya Young Africans.

Tahadhari kubwa iko kwa mchezaji Ibrahim Ajibu, ambaye ana kadi tatu za njano, hivyo kama atapewa kadi nyingine kwenye mchezo dhidi ya Majimaji, atakosa mechi ya Young Africans.

Ajali ya basi yaua 12 Njombe.
Audio: Wema Sepetu - Sitaki kusikia 'team' Wema, Asema kama wanapenda wakamsapoti Idris