Kikosi cha Young Africans kimewasili salama mjini Shinyanga, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC utakaochezwa kesho (Desemba 12), Uwanja wa CCM Kambarage.

Young Africans waliondoka Dar es salaam jana mchana kupitia jijini Mwanza kwa usafiri wa ndege na kisha walichukua usafiri wa basi hadi mjini Shinyanga.

Kocha Mkuu Cedric Kaze, amesema wachezaji wake wapo katika hali nzuri, na leo jioni watafanya maandalizi ya mwisho kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, tayari kwa mchezo wa kesho ambao ameutabiria kuwa na ushindani mkubwa.

Amesema kwake anahitaji kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi, lakini kwa wenyeji wao (Mwadui FC) watahitaji kushinda nyumbani hasa ikizingatiwa wamekua na matokeo mabaya msimu huu.

Kaze amesema kila mchezo kwao ni sawa na fainali na kila mchezaji anafahamu ‘kiu’ ya ubingwa waliyonayo na pamoja na kusaka tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Katika mchezo wa kesho Young Africans watakosa huduma ya kiungo kutoka nchini Angola, Carlos Calinhos ambaye bado ni majeruhi.

Young Africans ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 34 baada ya kushuka dimbani michezo 14 wakati Mwadui FC wenye alama 10 wako katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi hiyo na Ihefu FC inaburuza mkia.

Rais Magufuli afanya uteuzi
Kocha Mwadui FC aitangazia vita Young Africans