Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi ametangaza hali ya hatari kuelekea mchezo wa Mazunguuko wa 15 wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC.

Young Africans itacheza ugenini mkoani Lindi katika Uwanja wa Majaliwa kesho Jumatano (Desemba 07), ikihitaji kuendeleza wimbi la ushindi ili kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Kocha Nabi ambaye anaendelea kutumia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu amesema, dhamira ya kikosi chake kwa sasa ni kutofanya mzaha kwenye mchezo wowote ulio mbele yao, hivyo suala la ushindi linatangulizwa mbele na mengine yanafuata.

“Hatutafanya mzaha katika kila mchezo ulio mbele yetu, tukianza mchezo ujao tutakaocheza dhidi ya Namungo FC, ni lazima tupate ushindi ili tuendelee kukaa kileleni.”

“Nimewaona na kuwafuatilia Namungo FC katika michezo waliocheza siku za karibuni, nimebaini mambo mengi yanayowahusu, tutalazimika kuyatumia ili kupaata ushindi kwenye mchezo wetu wa kesho.” amesema Nabi

Katika hatua nyingine Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ameethibitisha wachezaji watatu wa Kikosi cha Kwanza cha Younga Africans Fiston Mayele, Jesus Moloko na Dickson Job watakuwa sehemu ya kikosi chake dhidi ya Namungo FC kesho Jumatano.

Wachezaji hao walikosa mchezo uliopita kwa sababu mbalimbali, lakini bado Young Africans ilipambana dhidi ya Tanzania Prisons na kuambulia ushindi wa 1-0, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Nina furaha kuwaona wachezaji wangu watatu muhimu ambao walikosekana kwenye mchezo wetu dhidi ya Tanzania Prisons wakirejea kikosini, ninaamini watapambana kwa kushirikiana na wengine ili kufanikisha kilichotuleta hapa Lindi.” amesema

Young Africans inaongoza msimaamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 35 sawa na Azam FC, huku Simba SC ikiwa nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 34.

Namungo FC ambayo rasmi kesho itamaliza mzunguuko 15 wa Ligi Kuu ipo nafasi ya tisa ikiwa na alama 18.

Awasilisha ombi la kisheria kusitisha mashitaka
Dkt. Kiruswa asitisha uchimbaji madini kwenye makazi ya watu