Imeelezwa kuwa Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans chini ya Kocha Mkuu Nasreddine Nabi, limeshtukiwa uwepo wa mashushushu wa US Monastir waliotua Dar es salaam.

Young Africans itaanza kampeni ya kusaka nafasi ya kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho kwa kuikabili US Monastir ya Tunisia mwishoni mwa juma hili (Februari 12), kwa kucheza ugenini.

Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa, kutokana na kushtukia mbinu za warabu hao waliotua nchini tangu juma lililopita, Kocha Nabi kwa kushirikiana na wasaidizi wake ameamua kikosi chake kucheza katika kiwango cha kawaida ili kuwapumbaza watu hao waliotumwa kufanya kazi ya kujua baadhi ya mbinu za kikosi chake.

Taarifa hizo zimeongeza kuwa, Kocha huyo kutoka nchini Tunisia ameamua kutumia mkakati huo, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC, ili kuharibu mipango ya wapinzani wao, ambao wanaonesha kujipanga kushinda mchezo wa nyumbani.

“Kumekuwa na malalamiko kwamba timu haichezi kwenye kiwango chake, lakini siyo kama Wachezaji au Benchi la Ufundi halijui chochote ila wamejua kuwa wapinzani wetu kutoka Tunisia wametuma maofisa wao wamekuwa hapa kufuatilia michezo yetu.”

“Alichokifanya Kocha ni kuangalia kwamba timu inaweza kupata matokeo katika kila mchezo bila ya kuangalia kiwango kipoje, kwa kuwa US Monastir wapo hapa wakifuatilia michezo yetu na kuona namna gani wanaweza kutuzuia, ila kilichofanyika ni kuwapoteza wao na kujua mifumo yetu ipo vipi Uwanjani. amesema mtoa taarifa hizi ambaye hakutaka jina lake kuandikwa Mtandaoni

Young Africans imepangwa Kundi D sambamba na Klabu za US Monastor ya Tunisia, TP Mazembe (DR Congo) pamoja na Real Bamako (Mali).

Bungeni: Kampuni za simu zatakiwa kufidia wateja
Simba SC kuifuata Horoya AC kimafia