Kufuatia hatua ya rapa wa Marekani, 50 Cent kufanikiwa kuuza msemo wake ‘Get the Strap’ kwa $1 milioni, Young Killer amefunguka kuhusu uwezekano wa kuuza msemo alioupa umaarufu wa ‘Pambana na Hali Yako’.

Rapa huyo kutoka jiji la miamba Mwanza, aliuweka msemo huo kwenye ngoma zake kadhaa nzito ikiwa ni pamoja na ‘Unaionaje’ aliyomshirikisha Harmonize. Msemo huo ulishika kasi kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi mitaani.

Akifunguka hivi karibuni, Killer alisema kuwa kuna ugumu wa kuuza msemo kama huo kwa Tanzania kwani hata unayemuuzia anaweza asiwe na njia bora ya kujihakikishia kuwa utamuingizia faida kwenye biashara yake.

“Sijafikiria, lakini maneno yetu hayahaya ndio huwa tunayageuza yanakuwa hela. Na kibongobongo pia ni ngumu. Unataka umuuzie nani?” Alihoji kwenye Misele ya Simulizi na Sauti.

“Na hata huyo ambaye unaweza kusema labda ukamuuzie msemo na yeye hawezi kujua kama huo msemo unaweza ukafanya vizuri au usifanye vizuri. Kwamba utakuwa ni habari nyingine na awekeze pesa yake kwako kwamba utakuja kuwa hatari huu msemo hapo ndipo kazi ilipo,” aliongeza.

Rapa huyo ambaye hivi karibuni ameachia ‘Hunijui’ akiwa amewashirikisha Dully Sykes na Ben Pol amefafanua kuwa yeye anajivunia tu kuwa sehemu ya watu waliotoa msemo unaoongeza chachu kwenye lugha adhimu ya Kiswahili na kutumiwa na watu wengi zaidi.

Wazo hilo linanifanya nivute kumbukumbu ya miaka mitano iliyopita ambapo Mtangazaji wa kipindi cha Milazo 101 cha Radio One wakati huo, Sandu ‘Kidbwoy’ Mpanda alipotaka kufahamu kutoka kwa AY kama itatokea kampuni ya simu ambayo ingenyakuwa msemo wa ngoma yake na Fid Q ‘Shimo Limetema’ na kuingiza kwenye biashara yake ya huduma za simu.

AY alijibu kuwa makampuni ya simu wanajua yeye ni mtu ‘smart’ na hivyo ni vigumu kwao kuchukua tu msemo alioupa umaarufu wakati huo na unaobeba wimbo wake na kuufanyia biashara bila makubaliano.

Furahia ‘Hunijui’ ya Handsome Boy asiye na Matunzo:

Bieber amchumbia Mwanamitindo Hauley Baldwin
Watoto nane kati ya 12 waokolewa wakiwa hai Thailand

Comments

comments