Rapa Young Killer Msodoki amekubali kwa masharti wazo la Nay wa Mitego kuhusu kurejea kwa aliyekuwa msimamizi wake wa muziki, Mona Gangster ambaye ni Bosi wa studio za Classic Sound.

Nay aliwasha moto kwa baadhi ya wasanii ikiwa ni pamoja na Young Killer kupitia wimbo wake ‘Fire’, akidai kuwa tangu waondoke kwa wasimamizi wao waliowatambulisha vizuri kwenye ulimwengu wa muziki, hawafanyi vizuri kama awali huku akidai tatizo kubwa ni ukosefu wa nidhamu kwa wasanii hao.

Akijibu mashambulizi ya Nay jana kupitia Friday Night Live ya East Africa TV, Young Killer alimnyooshea kidole Nay akidai alitoa kauli hiyo huku akiwa amesahau kuwa na yeye tangu aondoke kwa ‘Mr. T-Touch’ hajawahi kutoa wimbo ukawa ‘hit’ kama zamani.

“Kama Nay anataka mimi nirudi kwa Mona Gangster, na yeye arudi kwanza kwa Mr T-Touch. Kwa sababu tangu naye aondoke kwa T hajawahi kutoa hit-song ,” alisema Young Killer.

Alipotajiwa wimbo wa ‘Wapo’ wa Nay wa Mitego ambao ulishika vichwa vya habari na hata wasiofuatilia muziki waliujua, alidai kuwa nguvu ya wimbo huo haiwezi kufanana na wimbo kama ‘Muziki Gani’ alioutoa akiwa kwa Mr. T-Touch.

Killer ameachia wimbo wa ‘True Boya’ wenye dakika mbili kujibu diss ya Nay wa Mitego aka True Boy kwenye ‘Fire’. Ingawa sio wimbo rasmi, Msodoki ameruhusu vyombo vya habari kuucheza kama wimbo wa kawaida.

Trump awatolea uvivu Korea Kaskazini, ‘imetosha’
Ujerumani yahalalisha ndoa za jinsia moja