Na Somoe Ng’itu, Dar es salaam

Kiungo wa Mcameroon wa Coastal Union, Youssoufa Sabo amesema kuwa kiwango chake ni cha juu na anastahili kuzichezea timu kongwe za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam, Simba au Yanga zote za Dar es Salaam.

Sabo aliifunga bao la pekee la Coastal Union katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Ranzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambayo ilivunjika huku Yanga wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Akizungumza mwishoni mwa juma lililopita, Sabo ambaye aliwahi kufanya mazoezi Yanga, lakini Pluijm alimuacha alisema kwamba ameiva na makocha wa timu za ligi kuu Bara wameona uwezo wake.

“Najua pale nilipokuja hawakuamini, lakini nashukuru nimewaonyesha mimi nina uwezo gani, niko tayari kuzungumza nao kama wataniita,” alisema.

Hata hivyo, alishangaza Yanga kutolewa katika mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly, akisema yeye anaweza kujiunga na klabu yoyote watakayokubaliana ili kuitumikia katika msimu ujao.

Baada ya mechi kumalizika, Pluijm alimuita Sabo na kuzungumza naye. Hata hivyo Pluijm alikataa kueleza mazungumzo yake na kiungo huyo yalihusu nini. “Siwezi kukwambia tulichokuwa tunazungumza na kuhusu kiwango chake pia siwezi kusema lolote, mimi nilikuwa makini kufuatilia wachezaji wangu tu, ila kumbuka kila mchezaji Tanzania angependa kuchezea Yanga,” Pluijm alisema.

Sabo pia alifunga bao katika mechi ya robo fainali ya mashindano hayo dhidi ya Simba.

Tayari Azam FC imetinga fainali ya mashindano hayo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF) hapo mwakani.

BANDARI YA DAR KUUNGANISHA SINGAPORE NA EAC
SERIKALI YAZUIA UINGIZAJI HOLELA WA MCHELE