Hatimaye Kocha Mkuu wa zamani wa Young Africans Mwinyi Zahera, amefunguka baada ya Kiungo Mshambuliaji Ibrahim Ajibu, kuwa gumzo kufuatia kuisaidia klabu yake ya Simba SC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC.

Ajibu aliingia Uwanjani kipindi cha pili katika mchezo huo, alionesha uwezo wa ajabu na kupelekea kupatikana kwa mpira wa adhabu, baada ya kuchezewa hivyo na beki wa Namungo FC Haruna Shamte dakika za lala salama, ambapo hatua hiyo iliisaidia Simba kupata bao la ushindi lililofungwa na Meddie Kagere.

Zahera amesema sababu kubwa ya Kiungo huyo kuonekana lulu wakati wa utawala wake katika Benchi la Ufundi la Young Africans, ilitokana na kumpa msukumo wa kuaminisha ana ubora wa kucheza soka na kubadilisha matokeo wakati wowote.

Amesema Ajibu ana asili ya uvivu wa kujituma anapokua mazoezi na hata katika michezo ya ushindani, hivyo ilimchukua muda mwingi kukaa naye na kumwambia ukweli wa uwezo wake kisoka.

“Ni sawa na ukiwa na watoto watatu nyumbani mmoja akawa mvivu unaweza kumsusa?”

“Ni kitu ambacho hakiwezekani kwa upande wangu, niliwezana na mchezaji huyu kwa sababu muda mwingi nilikua nakaa naye na kumuambia yeye ni bora. Ukikaa na Ajibu na kumwambia nini anatakiwa afanye ni muelewa.” amesema Zahera

Mchezo dhidi ya Namungo FC ulikua wa kwanza kwa Ibrahim Ajib kuitumikia Simba msimu huu 2021/22, huku Mashabiki wakimpigia upatu wa kutaka awe sehemu ya kikosi kitakachokua kinaanza, kufuatia udhaifu ulioonekana kwenye kikosi chao katika baadhi michezo iliyowakabili.

RC Makalla afunga mafunzo ya vijana 628 wa Jeshi la akiba Dar es salaam
Serikali yaondoa tozo Sekta ya Uvuvi