Kiungo mshambuliaji mpya  wa Mbeya City fc , Zahor Pazzy  amemshukuru rais wa shirikisho la kabumbu nchini Jamal Malinzi kwa kufanikisha  kupatikana kwa hati yake ya uhamisho (ITC)  iliyokuwa imekwama  nchini DR Congo kwa miaka  miwili.

Akizungumza  mara baada ya kumalizika kwa mazoezi  ya leo kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, Zahor amesema kuwa anafuraha kubwa kuona amerudi rasmi kwenye  ulimwengu wa soka baada ya kukaa nje  kwa miaka miwili,  licha ya jitihada kubwa alizokuwa akizifanya.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu, hakika natanguliza sifa kwake, nimekuwa nje ya soka la ushindani kwa miaka miwili sasa, mara kadhaa nimejaribu kufanya jitihada za kuhakikisha naokoa kipaji changu lakini sikufanikiwa,” alisema.

“Namshukuru rais wa TFF amefanikisha  ndoto zangu za kuendelea kucheza mpira. Niseme wazi  kuna wakati nilikata tamaa kabisa, ingawa pia niliendelea kujipa moyo na kumuomba Mungu, nashukuru sasa niko huru na naweza kuitumikia timu yangu mpya,” aliongeza.

Mchezaji huyo pia aliwashukuru viongozi wa Mbeya City  Fc kwa kumpa nafasi ya kuitumikia timu hiyo licha ya kutokuwa kwenye soka la ushindani kwa muda mrefu. Alisema kuwa anaamini kwa jitihada za wachezaji na uongozi wa timu hiyo, wataibuka na ushindi dhidi ya Mbao FC, Jumamosi hii.

 Alitoa wito kwa wachezaji wenzake kuwa makini katika masuala ya usajili na uhamisho ili wasikutwe na majanga yaliyomkwamisha kwa miaka miwili.

Ndoto ya Lema kuwa nje ya gereza mwaka huu yayeyuka
Azam FC yawatema makocha wake