Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa zaidi ya sh. bilioni 500 zimelipwa kwa wakulima wa korosho kati ya sh. bilioni 700 zinazotarajiwa na kwamba malipo hayo bado yanaendelea kulipwa kwa wakulima wengine waliosalia.

Amesema kuwa tamko la Rais Dkt. John Magufuli la kwamba Serikali itanunua korosho kwa bei ya sh. 3,300 ni kwa ajili ya korosho za daraja la kwanza na bei ya korosho za daraja la pili ni asilimia 80 ya zile za daraja la kwanza.

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka.

Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho ambao walikuwa wakilipwa sh. 2,600 kwa kilo wakati Rais Dkt. Magufuli alisema Serikali itanunua kilo moja ya korosho kwa sh. 3,300.

“Malipo yanaendelea na sehemu kubwa ni kwa wakulima wenye kilo zaidi ya 1,500, Serikali itanunua korosho zote kama ilivyoelezwa. taratibu zinazofanyika ni kuhakikisha anayelipwa ni muhusika, wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu.”amesema Majaliwa

Aidha, amesema kuwa ilikuwa ni lazima kwa Serikali ifanye uhakiki kwa wakulima hususani wale wenye kilo zaidi ya 1,500 ili kujiridhisha kama ni wakulima, hivyo baada ya kuhakikiwa wakulima wote watalipwa fedha zao.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Januari 27, 2019 alitoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wahakikishe hadi Februari 15 mwaka huu wawe wamekamilisha zoezi la uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho.

TFF hakikisheni tunaibuka na ushindi AFCON- Majaliwa
RC Songwe aagiza mwenye kitambulisho asisumbuliwe