Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili inapokea wagonjwa wa moyo zaidi ya 200 kila wiki kutoka maeneo tofauti nchini na wengine ambao wameshapitia hospitali kwa matibabu ya hatua za mwanzo.

Taarifa hiyo imetolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi hiyo ya Moyo, Sulende Kubhoja alipokua akizungumza na Dar 24 Media katika mahojiano ya kipindi cha Afya Tips hususani swala la tundu kwenye Moyo.

Kubhoja amesema kwa siku moja taasisi hiyo huweza kupokea hadi wagonjwa 30 wenye matatizo ya moyo wakiwemo watoto chini ya umri wa miaka 18 ambao wanahitaji huduma za kitaalam zaidi katika swala la Moyo.

Katika kuelezea sababu za kuongezeka kwa matatizo ya Moyo Kubhoja amesema ni tatizo linaloanzia kwenye ubebaji wa Ujauzito ambapo watu wengi hawapimi afya zao kabla ya ujauzito hali inayopelekea kiumbe anaetungwa tumboni kukutana na shida za mama na kuunganishwa hasa kwenye moyo wake ambao ndio sehemu inayobeba uhai wa kiumbe.

Dk Kubhoja ameongeza kuwa kwa mazingira ya sasa hasa swala la utandawazi wanadamu wanabeba matatizo mengi ya kiafya bila kujijua, na hivyo kupelekea mwili kushindwa kulinda kiumbe kinachojengeka tumboni.

Akitoa ushauri wake wa jinsi ya kujikinga na magonjwa mengi ya kuzaliwa nayo na kijenetiki Dk Kubhoja amesema kabla ya kuamua kuanzisha familia na kubeba ujauzito ni vizuri watu wapime afya zao na kujitibu matatizo watakayokutana nayo na sio kubeba ujauzito na kuanza kutafuta wataalam wakati kiumbe kimeshaumbika tumboni.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) zilizotolewa mwaka 2011, vifo vilivyotokana na magojwa ya moyo nchini Tanzania vilifikia idadi ya watu 19,083 au asilimia 4.33 ya idadi ya vifo vyote. Na takwimu hizo zilionyesha idadi ya wanaofariki ni watu 117.64 kati ya watu 100,000. Takwimu hizi zinaiweka Tanzania katika nafasi ya 87 duniani kati ya nchi karibu 200.

Naibu Waziri atoa onyo kwa maafisa ardhi
Matumaini mapya kwa wachimbaji wadogo