Vyombo vya usalama nchini Kenya na Zambia, kwa nyakati tofauti vimewakamata raia wa China kwa tuhuma za kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Hatua hiyo ilianzia nchini Zambia wiki iliyopita, ambapo Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuwa linawashikilia raia wawili wa China kwa kosa la kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wafanyakazi wa kampuni moja ya ulinzi, katika jiji la Livingstone.

Baadhi ya wananchi wa Zambia pia walikamatwa wakihusishwa na tuhuma hizo, ambapo jeshi hilo lilieleza kuwa lilikamata bunduki na silaha nyingine za moto.

Kwa upande wa Kenya, Ijumaa iliyopita, Idara ya Uhamiaji iliripoti kuwa iliwakamata raia watano wa China wakiwa na vitu ambavyo vinaaminika kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa.

Kundi hilo la Wachina ambalo mmoja wao alikuwa mwanamke, linashikiliwa na polisi jijini Nairobi wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea.

“Vitu ambavyo walikutwa navyo ni pamoja na Radio Calls (simu za upepo), sare za jeshi, laptops, vinasa sauti na vinasa chuma. Wataendelea kushikiliwa kwa muda wakati ambapo vyombo vya usalama vinaendelea na uchugnuzi,” imeeleza Tweet ya Idara ya Uhamiaji ya Kenya.

Wiki kadhaa zilizopita, Kenya iliwakamata na kuwatimua raia kadhaa wa China waliobainika kujihusha na kazi ambazo ziko kinyume na sheria za nchi hiyo. Baadhi yao walikutwa wakijihusisha na biashara haramu ya ukahaba.

Mfanyabiashara mmoja wa Kichina pia alifukuzwa kutokana na kauli zake za ubaguzi, baada ya kudai kuwa Wakenya wote ni ‘nyani’.

 

Video: Dkt. Bashiru ahesabiwa siku CCM, Raia wawili wa China watimuliwa nchini
Video: Khabib ampiga McGregor, vurugu kubwa zaibuka ulingoni