Timu ya Judo Zanzibar imerejea visiwani wakitokea Bunjumbura Burundi wakishinda nafasi ya pili katika mashindano ya kumi ya Afrika Mashariki yaliofanyika huko.

Zanzibar wameshinda nafasi ya pili katika mashindano hayo ambapo wamefanikiwa kuibuka na Medali za dhahabu 2, fedha 1 na shaba 2.
Walioshinda Medali hizo kwa Zanzibar ni Hafidh Makame alishiriki Judo chini ya kilo 73 ambapo alishinda Dhahabu, na Masoud Kombo pia ameshinda Dhahabu akishiriki Judo chini ya kilo 100.

Wengine walioshinda medali wakitokea Zanzibar ni Mohammed Abdul rahman akishinda medali ya Fedha ambapo kashiriki judo ya juu ya kilo 100 na Abdul rabi Alawi yeye ameshinda fedha judo chini ya kilo 66.

Na mwana mama pekee aliotokea Zanzibar katika mashindano hayo Salma Omar amerudi na medali ya shaba akishinda chini ya kilo 52.

Burundi waliongoza katika Mashindano hayo ambapo walishinda medali za dhahabu 3, fedha 5 na shaba 3.

Yussuf Thabit Mbalambula ambae ni meneja katika msafara wa timu hiyo ya Zanzibar alisema kuwa mashindano yalikuwa magumu sana na pia wanashukuru wamerudi salama Zanzibar.
“Ukweli mashindano yalikuwa magumu sana, lakini vijana wangu wamepigana na tumefanikiwa kushinda nafasi ya pili, pia tunawashukuru sana wenyeji wetu Burundi walitupatia ulinzi mkubwa sana, maana hatari sana kulikuwa kule, lakini tulilindwa sana tunawashukuru Balozi wetu wa Tanzania nchini Burundi katupa ushirikiano mkubwa sana”. Alisema Thabit.

Katika mashindano hayo yalijumuisha nchi 4, wenyeji Burundi ambao walishinda nafasi ya kwanza, Zanzibar nafasi ya pili, nafasi ya tatu ilishikwa na Kenya na mwisho ilikamatwa na Ethiopia ambapo jumla ya washiriki wote ni 62 katika mashindano hayo ambapo wenyeji Burundi walishiriki 33, Zanzibar 8, Kenya 20 na Ethiopia mshiriki 1 pekee.

Kutoka Zenji: Soka La Zenji Bado Ni 'Kitahanani', Limeanza Kama Masihara hadi mahakamani
Picha: Dk. Slaa afunga pingu za maisha na Josephine Mushumbusi