Wananchi Visiwani Zanzibar wameendelea na shughuli zao za kila siku, hali iliyoashiria kutokuwepo taharuki kubwa iliyoripotiwa hivi karibuni kufuatia Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi uliofanyika.

Ripoti kutoka visiwani Zanzibar zimeeleza kuwa wananchi wameendelea kufanya shughuli zao za kila siku hususan katika eneo maarufu la Darajani na maeneo mengine, hali inayoashiria kurejea kwa utulivu wa kawaida katika visiwa hivyo.

Wakati utulivu huo ukiendelea kuongezeka, Mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameendelea kupinga uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi huo akidai kuwa ni uamuzi binafsi na kwamba ZEC inapaswa kuendelea na kazi yake ya kuhakiki matokeo na kumtangaza mshindi.

Maalim Seif ameelezea uamuzi waliopanga kuuchukua kama Chama endapo uamuzi wa kufuta matokeo hautaondolewa.

“Nafasi ya juhudi hizi za Kidemokrasia tunaangalia kama zitafanikiwa au hazitafanikiwa, ikiwa hazikufanikiwa kwa muda fulani basi sisi tushapanga hatua kadhaa ambazo tutachukua moja baada ya moja lakini ili mradi haki ya wananchi irudi. Hiyo haina compromise, ifahamike haki ya wananchi lazima irudi,” alisema Maalim Seif.

Wagombea urais wa vyama vingine vya upinzani wameuunga mkono msimamo wa Maalim Seif Sharif Hamad na kuitaka Tume hiyo kuendelea na zoezi la uchaguzi.

Ubalozi wa Marekani na Uingereza pamoja na waangalizi kutoka ‘Common Wealth’ wameendelea kumsihi Mwenyekiti wa ZEC kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa ZEC, alitangaza kuufuta uchaguzi huo kwa madai kuwa haukuwa wa huru na haki kufuatia mapungufu zaidi ya tisa yaliyojitokeza.

Lembeli Aeleza Hatma Yake Baada Ya Kushindwa, Ajibu Tetesi Juu Yake
Dkt. Magufuli Atangazwa Rasmi Kuwa Mshindi Urais, Kinana Azungumza