Ziara ya waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa mjini Bukoba mkoani Kagera iliyolenga kuwafariji waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani humo jana ilizua gumzo baada ya umati mkubwa wa wananchi kujiunga huku polisi wakionekana kuweka ulinzi mkali kwa silaha na mabomu ya machozi.

Lowassa ambaye aliongozana na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Hamisi Mgeja aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamia Chadema akimfuata Lowassa alifika katika mitaa mbalimbali iliyoathirika tetemeko hilo na kuzungumza kwa ufupi na wananchi.

“Ninawapenda… poleni kwa matatizo, asanteni kwa kunipa kura,” alisikika Lowassa. “Nimekuja kuwapa pole na mchango wangu nitauwasilisha kwa mkuu wa mkoa,” aliongeza.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi liliuvunja mkutano wa ndani uliokuwa ukiandaliwa kwa ajili ya Lowassa na viongozi wa Chadema wa mkoa huo katika ukumbi wa St. Theresa huku umati mkubwa wa wananchi ukionekana katika jengo hilo.

Baada ya kuwapa pole waathirika hao, Lowassa na msafara na viongozi wengine walikutana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu na kumkabidhi msaada wa mifuko 400 ya saruji.

Pamoja na mambo mengine, Lowassa alifikisha kilio chake kwa mkuu wa mkoa huyo akilaani kitendo cha jeshi la polisi kubeba mabomu ya machozi kwenye msafara wake wa amani akidai kitendo kile ni kutishia wananchi na kwamba huu sio wakati wa uchaguzi.

Naye Mbunge Lwakatare alilalamikia kitendo cha jeshi la polisi kuvunja mkutano wa ndani wa Lowassa na viongozi wa Chadema akidai kuwa kama wangeona kuna watu wengi, wangewasiliana nao ili waone namna ya kuwaondoa wasiohusika na kikao hicho.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huo hakujibu malalamiko hayo lakini aliwafafanulia kuhusu hali ilivyo hivi sasa kutokana na janga hilo na changamoto wanazokabiliana nazo kuwasaidia waathirika ambayo ni kati ya mambo waliyoomba kupewa ufafanuzi.

Lowassa alishauri Serikali kuchukua hatua stahiki kwa uharaka zaidi kwani madhara aliyoyaona ni makubwa kuliko watu walivyofikiria.

Watumishi wa Umma watakiwa kuwa tayari kufanya kazi kokote nchini
Video: DC Mgandilwa kuimarisha usalama kigamboni, Vituo vya Polisi kujengwa