Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limesema kuwa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad katika mkoa huo imeleta madhara makubwa na kuongeza matukio ya kihalifu na uadui wa kisiasa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Mohamed Sheikhan Mohamed aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa baada ya ziara ya Maalim Seif aliyoifanya Mei 17 mwaka huu, matukio mengi ya kihalifu yalitokea na kuripotiwa katika vituo mbalimbali vya Polisi lakini ushughulikiaji wake umekuwa na changamoto.

Alisema kuwa Maalim Seif aliwahamasisha wanachama wa CUF kufanya migomo kwa vitendo na kutoshirikiana na wananchama wa CCM, kauli iliyoleta matokeo ya kihalifu baadae.

Akitaja baadhi ya matukio yaliyoripotiwa, alisema wanachama wawili wa CUF (Abdallah Mussa Hamad na Mussa Abdallah Said walimshambulia Ali Omar Mrisho kwa ngumi wakimzuia kuingia msikitini kwakuwa ni mfuasi wa CCM.

Matukio mengine ni kuchomwa moto kwa nyumba, kuharibu mashamba ya watu wanaoamini kuwa ni wafuasi wa CCM.

Kamanda Mohamed alisema kuwa jeshi hilo limekuwa likikumbana na changamoto ya upelelezi kwa kukosa ushirikiano wa wananchi katika kutoa ushahidi kwani wengi ni wafuasi wa CUF.

Alisema kuwa Jeshi hilo limejidhatiti kufanya doria kwa miguu na magari kupambana na vikundi vya kihalifu katika maeneo hayo na kuwafikisha mahakamani wote wanaobainika kuhusika katika vitendo vya kihalifu.

Vuguvugu hilo ni sehemu ya madhara ya mtafaruku wa kiuchaguzi kati ya CCM na CUF, hususan baada ya CUF kususia uchaguzi wa marudio wakipinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.

Mmiliki Wa TP Mazembe Ahukumiwa Kifungo
Magufuli ashusha nyundo 7, apasua makampuni ya madini, Mafao hewa, miamala ya simu