Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempa siku tatu kaimu muweka Hazina wa wilaya ya Itigi, Optatus Likiliwike ahakikishe anarejesha sh. milioni 1.6 ambazo alijilipa posho kinyume cha utaratibu.

Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Manyoni ambao wanajumuisha halmashauri za wilaya za Itigi na Manyoni.

” Kabla sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione ‘pay in slip’ kuthibitisha kuwa fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki niione hiyo pay in slip kabla sijaondoka.” amesema Waziri mkuu

“Wewe si ndiye Otto au Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za fedha zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?,” alihoji  Waziri Mkuu.

Muweka hazina huyo amejitetea kwa kusema “Nilichukua fedha lakini kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa naenda wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma,” alijibu Likiliwike.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka afisa huyo arejeshe sh. milioni 196 za ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.

“Hizi fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za retention, ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi nyingine?” Waziri Mkuu alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina waliokuwepo kabla yake.

Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Bw. John Mgalula ambaye aliteuliwa wiki iliyopita asimamie marejesho ya posho za Bw. Likiliwike pamoja na marejesho ya sh. milioni 196 ambazo mweka hazina huyo ameahidi kuwa Halmashauri yake imetenga sh. milioni 70 ili zirejeshwe kila mwaka.

Likiliwike ametolea ufafanuzi kwamba fedha zinazodaiwa kutumika zilikuwa zimetumwa na Hazina kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini zililazimika kuchotwa na uongozi uliopita ili zitumike kuweka miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya ya Itigi.

Alisema waliohusika ukiukwaji huo ni Mkurugenzi aliyepita, Pius Luhende na Mweka hazina aliyepita Charles Mnamba. Hata hivyo, amekiri kwamba fedha hizo hazikuombewa kibali cha matumizi hayo.

Aidha amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo wahoji matumizi ya fedha hizo na wawaorodheshe wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo. “Kaeni na mkaguzi wenu wa ndani, awape taarifa juu ya matumizi hayo,” amesema.

Awali, Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni, Charles Fussi ahakikishe anarejesha mkopo wa sh. milioni 100 kutoka benki ya CRDB ambazo walikopeshwa madiwani.

Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa deni hilo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu na riba zinazotozwa na benki.

“Hakikisha unamaliza hilo deni la sivyo hawa Waheshimiwa hawatapata stahili zao hadi deni liishe. Pia unataka kusababisha mgogoro baina ya benki na Halmashauri.”

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.

Serikali yapiga marufuku ujenzi wa viwanda kwenye makazi ya watu
Meddie Kagere asukiwa mkakati wa kuihama Simba