Ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, January Makamba imepelekea kubainika kwa uwepo wa mafuta ya dizeli (diesel) kwenye visima vya maji mkoani Songwe.

Hayo yalibainishwa kupitia taarifa ya Mazingira ya Mkoa wa Songwe iliyosomwa na viongozi wa mkoa huo kwa Waziri makamba. Taarifa hiyo ilieleza kuwa mafuta hayo siyo mafuta ghafi yanayotakiwa kupatikana ardhini.

Pamoja na tatizo hilo, taarifa hiyo pia ilibainisha uvamizi wa binadamu katika vyanzo vya maji hali inayotishia uhai wa vyanzo hivyo.

makamba-3

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Makamba aliahidi kusaidia kuwapata wataalamu watakaoweza kutambua chanzo cha tatizo la uwepo wa mafuta hayo katika maji pamoja na njia sahihi za kukabiliana na tatizo hilo.

Ziara ya Makamba katika Mkoa huo pia ilifika katika wilaya ya Ileje ambapo alipokea taarifa ya mazingira. Waziri huyo alipongeza juhudi za wilaya hiyo katika utunzaji wa mazingira hasa eneo lenye msitu mkubwa ulioko wilayani humo.

Aidha, aliahidi kuzisaidia Halmashauri za Wilaya na Vijiji kupata namna sahihi na bora zaidi ya kuandaa sheria ndogo za mazingira ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa Mazingira.

Akiwa katika kijiji cha Lubanda, Makamba aliwasihi wananchi kutokata miti hovyo na kuacha kulima katika vyanzo vya maji. Aliwasisitiza kufanya kilimo cha matuta (kontua) katika miteremko ya milima ili kuepusha mmomonyoko wa udongo na rutuba hali inayoweza kusababisha ardhi kuzalisha kwa kipindi kifupi.

“Nikiwa njiani nimeona kuna uchepushaji wa maji, hii ni dhambi kubwa sana ya kimazingira na hatuna budi kuiacha na kufuata taratibu zilizowekwa kisheria za matumizi sahihi ya maji,” Waziri Makamba anakaririwa.

makamba-2

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira akiwaelekeza jambo viongozi wa Mkoa wa Songwe

Waziri Makamba amemaliza ziara yake katika Mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe na  anatarajia kuzuru mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na kumalizia ziara yake mkoani Dodoma.

Jaji lubuva aitakata tume haki za binadamu kuimarisha utawala bora
Picha: Maonyesho ya urembo 'Mr na Ms' Albino Kenya