Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba jana alitembelea mkoa wa Iringa ikiwa ni sehemu ya ziara yake mikoani, baada ya kumaliza ziara yake mkoani Morogoro.

Akiwa mkoani humo, Waziri Makamba alitembelea bwawa la Kuzalisha Umeme Kihansi na Maabara ya Chura wa Kihansi. Waziri alipongeza juhudi za uhifadhi wa mazingira kuzunguka eneo hilo ambapo wanapatikana chura wa kipekee duniani na pia ni moja kati ya vyanzo tegemezi vya nishati nchini.

Katika kutambua umuhimu wa eneo hilo Waziri Makamba ameahidi kuanza mchakato wa kutangazwa kwa eneo hilo kuwa eneo mahsusi ili kulilinda zaidi kisheria.

makamba-2

Aidha, Makamba pia alifika katika Kijiji cha Mwatasi, Wilaya ya Kilolo  ambapo alizungumza na wakazi wa Vijiji vya Mwatasi na Wangama pamoja na viongozi wa vijiji  hivyo, ambapo amepongeza kazi kubwa inayofanywa na vijiji hivyo katika utunzaji wa vyanzo vya maji ambavyo vinapeleka maji katika bwawa na Mto Kihansi pamoja na mto Kilombero. Katika kutambua mchango mkubwa wa kamati za Mazingira katika vijiji vya Mwatasi na Wangama, amezipatia kamati za mazingira za vijiji hivyo shilingi laki moja kwa kila kijiji ili kukuza na kufufua mfuko wa mazingira na kusaidia kuendeleza shughuli za uhifadhi.

makamba-3

Pia, Waziri Makamba amemwagiza kubakizwa kwa sehemu ya tozo ya faini ya uharibifu wa mazingira ili iweze kutumika katika kusaidia shughuli za Kamati ya Mazingira ya vijiji hivyo.

Kadhalika, alitembelea moja kati ya vyanzo vya maji na kushuhudia kilimo cha mbogamboga na miti ndani ya chanzo hicho, kinyume cha taratibu na sharia. Hivyo, Waziri aliagiza Serikali ya Wilaya/Halmashauri/NEMC kuhakikisha kuwa ndani ya wiki nne watu hao wawe wameondolewa, miti iliyopandwa katika chanzo cha maji ikatwe na chanzo kirejeshwe katika hali yake.

Waziri alipokea taarifa ya mazingira ya mkoa huo kabla ya kupata wasaa wa kufika katika kituo cha maji Ndiuka ambacho ndicho husafisha maji na kutibu maji toka mto mdogo Ruaha kabla ya kusambazwa kwa matumizi ya kila siku. Akiwa katika kituo hicho Waziri Makamba amepokea taarifa toka kwa Mkuu wa Mko wa Iringa, Amina Masenza juu ya uchafuzi wa Mazingira katika mto ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa Manispaa ya Iringa.

Aliagiza Jeshi la polisi pamoja na Mamlaka za Manispaa kushirikiana na NEMC kuweka ulinzi katika kingo za mto huo na kuwachukulia hatua watu watakaobainika kuhusika na uchafuzi huo.

Pamoja na mambo mengine, Waziri ameupongeza mkoa wa Iringa kwa jitihada zake katika uhifadhi na utunzaji wa Mazingira.

Taarifa ya mkoa huo imeonyesha kuwa kati ya mwaka 2012/2012 na 2015/2016 mkoa umefanikiwa kupanda miti takribani Milioni 60. Pia amepongeza juhudi za mkoa kutunza vyanzo vya maji ambapo kati ya vyanzo 2600 vilivyopo takribani vyanzo  1700 vimehifadhiwa.

Mwamuzi Anthony Taylor Amponza Jose Mourinho
Ronaldo de Lima Amfagilia Cristiano Ronaldo