Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa miradi mikubwa ya uwekezaji baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional Properties’  ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
 
Utiaji saini huo ambao kwa upande wa Zanzibar ulifanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Shariff Ali Shariff na kwa upande wa Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional Properties’ ulifanywa na Mohammed Ali Rashid Alabar. 


Mwekezaji huyo awali alimweleza Rais Dk. Mwinyi kuridhishwa kwake na mazingira ya uwekezaji Zanzibar ambapo ni tofauti na alivyotembelea katika mataifa mengine duniani ambako nako amewekeza miradi mikubwa.
 
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kumuunga mkono na kuahidi kwamba atafanya kila linalowezekana kuhakikisha uwekezaji anaotarajia kuufanya unafanikiwa.
 
Miradi inayotarajiwa kujengwa na mwekezaji huyo ni hoteli ya nyota tano eneo la Kizingo, Mjini Zanzibar ambapo pia, mwekezaji huyo anatarajiwa kujenga nyumba Zanzibar kwa ajili ya maeneo ya makazi.


 
Vilevile, chini ya mradi huo eneo jingine litakalonufaika na uwekezaji huo ni Matemwe katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambako kutajengwa hoteli yenye hadhi ya nyota tano pamoja na nyumba za kuishi zenye hadhi ya juu kwa ajili ya soko la watalii na watu wenye uwezo
 
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alihudhuria sherehe za kuwatunuku vyeti washindi wa  mpango endelevu wa Abudhabi unaojikita kuendeleza masuala ya afya,chakula, nishati, maji na  maendeleo ya elimu duniani sherehe iliyofabyika Dubai.
 
Rais Dk. Mwinyi katika shughuli nyingine aliyoifanya ni kutembelea banda la Tanzania katika maonyesho ya Kimataifa ya Dubai yanayojulikana kama ‘Expo 2020’.
 
Rais Dk. Mwinyi anaendelea na ziara yake katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ziara inayotarajiwa kumalizika Januari 19, 2022 na baadae kurejea nyumbani.

Mbuni FC kuipima Young Africans
Bocco: Kufunga ni mipango ya Mungu