Si unaikumbuka ile ziara ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, waliyofanya jijini Ndola Zambia mwezi uliopita? Sasa imeanza kuzaa matunda kwa mabingwa hao kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya Bidvest Wits ya huko.

Azam FC ikiwa na kikosi bora kabisa iliyofikia katika Hoteli ya kifahari ya Garden Court jijini Johannesburg itaumana na Bidvest Wits katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Bidvest Wits kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Mabingwa hao walifanya ziara hiyo waliposhiriki michuano maalumu ya timu nne, iliyohusisha timu nyingine za Zesco United, Zanaco FC ambao ndio walikuwa wenyeji pamoja na mabingwa wa Zimbabwe Chicken Inn, ambapo Azam FC ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz jana usiku Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliyeambatana na kikosi hicho jijini hapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Nassor Idrissa, alisema wanashukuru kukutana na hali ya hewa ya mvua na baridi waliyokutana nayo walipokuwa kwenye michuano maalumu Zambia.

“Kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kuwa timu imewasili salama na jana (juzi) kulikuwa na mvua kubwa na timu iliweza kufanya mazoezi kwenye hali ya mvua, utakumbuka kuwa hali hii ndio tuliikuta tukiwa Ndola (Zambia) na wenzetu wa Zesco United walituambia hii ndio hali mtakayoikuta Afrika Kusini mwezi wa tatu, kwa hiyo tunashukuru sana kwamba ni hali ambayo sio ngeni kwetu kwa sasa hivi, ni hali ambayo tumefanyia mazoezi na kuchezea mechi,” alisema.

Kawemba alisema kuwa jana wao pamoja na viongozi wa Bidvest Wits walifanya vikao pamoja na Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

“Kwa hiyo kwa maana ya mchezo kila kitu kinakwenda vizuri na tunaamini kabisa ya kwamba kesho (leo) ni siku ya mwisho ya mazoezi tutapata nafasi ya kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bidvest kwa sababu ndio uwanja wa mechi na baada ya mazoezi kutakuwa na kikao cha benchi la ufundi na hivyo kufanya taratibu za mchezo kuwa zimekamilika kwa ajili ya kuchezwa,” alisema.

Bosi huyo aliyebobea kwenye masuala ya uongozi wa soka, alichukua fursa hiyo kuwaomba Watanzania kuwa waendelee kuamini kwamba Azam FC ina uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Kwa maana ya timu tunamshukuru Mungu hatuna majeruhi yoyote na kwa maana ya maandalizi ya wenyeji wetu hapa kwa kweli kila kitu kinakwenda sawa na mpaka sasa hivi hakuna kitu chochote kinachokwenda vibaya dhidi yetu kwenye melengo yetu,” alisema.

Chanzo: Azam FC

Kocha Wa APR Atamba Kuwaadabisha Yanga Kesho
Rafael Benitez Kuwa Mbadala Wa Steve McClaren