Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe Dkt. Mhandisi Polite Kambamura na wataalamu wake wametembelea Viwanda vya kuchakata na kusafisha dhahabu nchini katika jiji la Mwanza.

Ziara hiyo ambayo imelenga kujengeana uwezo kuhusu Sekta ya Madini na kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi katika sekta hiyo.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akimkaribisha mgeni wake amesema wamekuja kujifunza namna bora ya uchimbaji, utafutaji, uongezaji thamani na biashara ya madini.

Akizungumza, katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited), Dkt. Kiruswa amesema, ushirikiano wa Tanzania na Zimbabwe kwenye Sekta ya Madini ni wa kujengeana uwezo kwa kuwa Zimbabwe imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya madini kupitia wawekezaji wakubwa.

Amesema, ujumbe wa Sekta ya Madini kutoka Zimbabwe unataka kujifunza namna gani Tanzania imefanikiwa katika kuwalea wachimbaji wadogo hadi kufanikiwa kuwatengenezea masoko ya madini ya kuuza na kununua hapa nchini.

Pia ameongeza kuwa ujumbe huo, utajifunza kuhusu fursa ya madini yaliyopo Tanzania, mfumo wa usimamizi wa leseni na usimamizi wa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe, Dkt. Mhandisi Kambamura amevutiwa na kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ambacho kinasafisha kiasi cha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa ubora wa asilimia 999.9.

Amesema, Tanzania ni nchi iliyofanikiwa kwenye Sekta ya Madini hususani kuwaendeleza wachimbaji wadogo jambo lililofanya waje kujifunza.

Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Deusdedith Magala akizungumza kwa niaba ya STAMICO amesema, kiwanda cha kusafisha dhahabu nchini itafanya wafanyabiashara wa Zinbabwe wavutiwe kupeleka dhahabu yao kwa ajili ya kusafishwa katika kiwanda cha Mwanza kutokana na kuwepo kwa mazingira wenzeshi ya uwekezaji hapa nchini.

Naibu Waziri wa Madini Zimbabwe na ujumbe wake wapo nchini kwa ziara ya siku tano na Katika ziara hiyo watatembelea mgodi wa dhahabu wa GGM, wachimbaji wadogo wa Nyarugusu na wachimbaji wadogo wa almasi wa Shinyanga.

Habari zilizojiri kwenye magazeti leo Mei 24, 2022
Songea yaonja matunda ya tiba Mtandao