Beki wa pembeni wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kikosi chao hakina budi kucheza kwa malengo kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.

Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo Januari 06 mwakani, huku ikiwa nyuma kwa bao moja kwa sifuri, baada ya kupoteza mjini Harare, Zimbabwe juma lililopita (Desemba 23).

Zimbwe Jr ametoa hamasa hiyo kwa wachezaji wenzake kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambapo ameandika: “Tunapaswa kucheza kwa malengo mechi ya marudiano dhidi ya FC Platinum, kama kweli tuna dhamira ya kufika mbali, vinginevyo yanaweza kutokea yale ya mwaka jana dhidi ya UD Song tukabaki tunamtafuta mchawi.”

Beki huyo alikua sehemu ya kikosi cha Simba SC kilichopoteza mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Harare, Zimbabwe na alionesha kujituma wakati wote.

Tayari Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC imeshatangaza kauli mbiu itakayotumika kuwahamasisha wachezaji na mashabiki kwenye mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Kauli mbiu ya mchezo huo ni War In Dar (WIDA), ikimaanisha Vita ndani ya Dar.

Simba SC itatakiwa kushinda mabao mawili kwa sifuri na kuendelea ili kujihakikishia safari ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, huku FC Platnum wakihitaji sare ama ushindi kufikia lengo la kuwatupa nje Mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Babu amtumia salamu Deus Kaseke
Djodi 'OUT' Azam FC