Ufungaji wa Kamera kwenye daraja la juu la Mfugale lililopo Tazara jijini Dar es salaam, unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 14, kufuatia Kamera 14 zilizokuwa zimebaki kuwasili nchini jana.

Mkuu wa kitengo cha manunuzi na mikataba cha wakala wa barabara Tanzania (Tanroads), Abednego Lyanga amesema kuwa hadi sasa kamera mbili zimesha fungwa na zilizobaki ni 14 ambazo zilitarajiwa kuanza kufungwa leo.

“Kamera mbili zilifungwa mwishoni mwa Januari mwaka huu na Kamera nyingine 14 zilikuwa bado, kampuni ya E1 ndiyo ilishinda zabuni ya kazi hiyo, kazi ya kuanza kufunga itachukua takribani wiki mbili, hivyo wiki ijayo huenda zikawa tayari ” amesema Lyanga

Pia amesema kuwa kamera hizo 16 zitakuwa zikionesha matukio yote yanayoendelea katika eneo hilo, na iwapo makosa ya usalama barabarani yatafanywa na madereva itakuwa rahisi kuwabaini na kuchukua hatua, na zitakuwa zinafanya kazi muda wote kuhakikisha miundombinu ya eneo hilo ipo salama.

Aidha, ikumbukwe kuwa agizo la kufungwa kamera hizo lilitolewa Septemba 27, 2018 na Rais Magufuli wakati akizindua daraja hilo na kusisitiza kuwa kamera hizo zitawabaini wanaoendesha vyombo vya moto bila kufuata taratibu wakiwemo walevi.

Hata hivyo, baada ya miezi mitatu kupita baada ya kutangazwa kwa zabuni na kushinda kampuni ya E1, Kamera mbili zilifungwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu na zilizo bakia zinatarajiwa kukamilika mwezi huu Machi.

 

Makamu wa Rais akutana na Watanzania waishio Uganda
Spika Ndugai amshangaa Lissu,' Huwezi kudai mshahara mitandaoni'