Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amewataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuuangalia kwa jicho la tatu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ili wasije kutunga sheria itakayosababisha kufutwa kwa chama chao siku za usoni.

Akitoa mchango wake leo ndani ya Bunge, Zitto alisema kuwa kifungu cha 19 C cha muswada huo, kinapaswa kuondolewa kwa sababu utaratibu wa kusajili chama cha siasa ulioelezwa utaigharimu CCM kwani kuanzishwa kwake hakukufuata utaratibu huo.

Akielezea kifungu hicho, alisema kuwa kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kukifuta chama chochote ambacho ataona kuwa mchakato wake wa usajili uligubikwa na udanganyifu (fraudulent).

“Kifungu hiki kifutwe kwa sababu hakina maana. Chama cha kwaza kufutwa kinaweza kuwa Chama Cha Mapinduzi.  Kwa sababu Chama Cha Mapinduzi hakikusajiliwa, hakikufuata mchakato  ambao vyama vingine vyote vya siasa vilifuata kwenye usajili. Kilitungwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Zitto Kabwe.

“Leo hii ninyi mko madarakani, mna majority ya Bunge. Kesho mkipoteza majority hata ya mbunge mmoja, kitendo cha kwanza cha kiongozi yeyote atakayeingia madarakani ni kwenda kuwafuta kwa sababu hamkufuata sheria… sasa mnajitungia sheria hata ya kuwanyonga ninyi wenyewe?” Alihoji.

Katika hatua nyingine, Zitto alieleza kuwa katika muswada huo, kuna vifungu ambavyo vimeandikwa vikilenga kuwadhibiti watu fulani, akikimulika zaidi kifungu kinachomkataza mtu ambaye mzazi wake mmoja sio raia wa Tanzania kuanzisha chama cha siasa.

“Tulikubaliana kwenye Kamati, mimi nilialikwa kama mgeni… kwamba rejea ya uraia itumike rejea ya uraia ya ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini ‘schedule of amendment’ imekuja, labda Mheshimiwa Jenista [Mhagama] aseme wamekosea… ni tofauti kabisa na lile ambalo lilikubaliwa ndani ya Kamati,” alisema.

“Eti kwamba leo, ukiwa umezaliwa na mzazi mmoja ambaye sio raia wa Tanzania, unaweza kuwa Rais, unaweza kuwa Mbunge, unaweza kuwa Waziri Mkuu lakini hauwezi kuanzisha chama cha siasa,” Mbunge huyo wa Kigoma Mjini aliongeza.

Aidha, alieleza kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya demokrasia na maendeleo na kwamba ukuaji wa demokrasia unaenda sambamba na ukuaji wa maendeleo ya nchi.

Awali, Kamati za Bunge zimefanyia kazi mapendekezo kadhaa na kubadili vifungu kadhaa vya muswada, ambavyo baadhi ya wachangiaji akiwemo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ameeleza kuyashuhudia.