Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati maalum ya Bunge iliyochunguza sakata la kukwapuliwa kwa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow amemshauri mazito Rais John Magufuli baada ya Tanesco kuamriwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni 320.

Hivi karibuni, mahakama ya inayoshughulika na migogoro ya uwezekaji (ICSID) yenye makao yake mjini Washington DC, Marekani ilitoa uamuzi dhidi ya mgogoro wa uwekezaji kati ya Tanesco, IPTL na Standard Chartered Bank-Hong Kong (SCB-HK), ikiitaka Tanesco kulipa kiasi hicho cha fedha.

Awali kiasi hicho cha fedha (sh bilioni 320) kiliwekwa kwenye akaunti maalum ya ‘Tegeta Escrow’ kwa lengo la kusubiri maamuzi ya kesi hiyo ili atakayeshinda apewe, lakini wakati kesi ikiendelea ilibainika kuwa vigogo kadhaa walizitoa fedha hizo na kugawana chini ya mmiliki wa IPTL/PAP, Harbinder Singh Seth kupitia benki kadhaa nchini.

Sakata hilo lilitua bungeni katika Serikali ya Awamu ya Nne na kupelekea baadhi ya mawaziri akiwemo Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu (japo ilithibitika hakupokea pesa yoyote ya mgao) huku Profesa Anna Tibaijuka akiondolewa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, vyombo vya habari vimemtafuta Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye amekaririwa akieleza kuwa hilo ni deni la Tanesco hivyo wao ndio wanapaswa kulitolea majibu.

Kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT – Wazalendo ameandika ushauri mrefu kwa Rais Magufuli akitaka awachukulie hatua kali wahusika.

Hivi ndivyo alivyoandika:

Kwanini Rais Magufuli hafanyii Kazi suala la IPTL?

Matapeli hawa wataendelea kuipa hasara Nchi yetu mpaka lini? Sasa mahakama ya ICSID imeamua kuwa Benki ya Standard Chartered ilipwe Shilingi za Kitanzania Bilioni 300 na riba. TANESCO wanaingia Hasara hii Kwa sababu ya wizi wa Fedha za TEGETA Escrow, na Rais bado anavuta miguu kuchukua hatua dhidi ya suala hili. Nini kimemkuta Rais Magufuli? Rais anataka tuamini kuwa IPTL/PAP Ni kweli waligharamia Mkutano Mkuu wa CCM uliompa yeye Uenyekiti ?

 Tanzania hapo ni hasara tupu:

1) Mmelipa matapeli Fedha zilizokuwa kwenye TEGETA escrow account

2) Mmewapa mtambo wa kuzalisha umeme matapeli hao na mnaendelea kuwalipa capacity charges mpaka sasa

3) Mnawalipa standard chartered Fedha zao Kwa mtambo ambao sio wenu na Kwa Fedha ambazo mngezitoa escrow a/c lakini sasa mtazitoa hazina

Rais achukue hatua zifuatazo

– Awafikishe mahakamani watu wote waliohusika na kuitia Nchi hasara katika sakata la TEGETA Escrow

– Aitwae mitambo ya IPTL kisheria na kuimilikisha Kwa TANESCO

– Amkamate Bwana Harbinder Singh Seth na wafuasi wake wote na kuwafikisha mahakamani Kwa makosa ya utapeli, wizi, uhujumu uchumi, utakatishaji wa Fedha nk

– Benki iliyotumika kupitisha Fedha za TEGETA escrow ndio ilipe Hilo deni tunalotakiwa kulipa

Rais aamue kusimama na watanzania au kusimama na matapeli wa TEGETA escrow.

SSC Napoli Wamfungia Milango Kalidou Koulibaly
Chadema wamtumbua Diwani wao kwa ufisadi