Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameitaka serikali kufikiria kubadilisha sheria ya uhamiaji, ili kuruhusu uwapo wa wachezaji wenye uraia wa nchi mbili kwa ajili ya manufaa ya michezo Tanzania.

Zitto amesema hata kama serikali haitaki kufanya hivyo kwa raia wote, lakini iangalie suala hilo kwenye nyanja za michezo kwa sababu nchi inapoteza wanamichezo wengi ambao ni Watanzania wenye uraia wa nchi zingine na wenye vipaji, ambao wangeweza kulipatia sifa taifa pamoja na mapato pia.

“Mfano kuna mchezaji mmoja anaitwa Yusuph Poulsen, huyu baba yake ni Mtanzania kutoka Tanga, huko nyuma aliwahi kusema kuwa kabla ya kucheza timu ya Taifa ya Denmark alikuwa anataka kuchezea timu ya Tanzania, Taifa Stars, lakini ikashindikana kutokana na kutokuwapo kwa sheria hiyo,” alisema kiongozi huyo.

Zitto amesema kwa sasa uraia pacha umekuwa ukizinufaisha sana nchi za Comoro, Madagascar na hata Cape Verde ambazo wachezaji wao wengi wamekuwa wakitoka nje ya nchi, lakini wenye asili ya nchi hizo na wamezibadilisha nchi hizo kutoka kuwa timu vibonde na sasa ni tishio kwenye soka la Afrika.

Banda: Mkude, ana uwezo wa kucheza Afrika Kusini
Kibu: Simu za viongozi Simba, Young Africans hazikauki