Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe leo ametoa maelezo mengine kuhusu azma yake ya kufungua kesi ya kikatiba kufuatia hatua ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumuita katika kamati ya Bunge Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Mwanasiasa huyo ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema kuwa amemuelekeza mwanasheria wake, Fatma Karume kufungua rasmi kesi leo ili Mahakama itoe tafsiri ya Ibara ya 143 (6) kuhusu kinga ya CAG.

“Licha ya vikwazo katika mahakama ya Tanzania, kwa masilahi ya umma, nimetoa maelekezo kwa mwanasheria wangu Fatma Karume kufungua kesi leo ili Mahakama itoa tafsiri ya kikatiba ya Ibara ya 143(6) juu ya kinga na uhuru wa CAG,” tafsiri isiyo rasmi ya tweet ya Zitto.

Zitto na Fatma jana walieleza kuwa Msajili wa Mahakama amekubali kuipokea na kuisajili kesi yao ikiwa ni siku moja baada ya kuwaandikia barua kuwa kesi hiyo haiwezi kupokelewa.

Kesi hiyo inafunguliwa ikiwa tayari CAG ameshazungumza na kueleza kuwa ana nia ya kufika mbele ya Kamati ya Bunge kwa maslahi ya kuboresha uhusiano kati ya ofisi yake na mhimili huo.

CAG alieleza kuwa neno ‘udhaifu’ au upungufu ni lugha ya kawaida inayotumiwa na ofisi yake pale ambapo kunakuwa na mapungufu.

“Maneno udhaifu au upungufu ni lugha za kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya mifumo na utendaji katika taasisi mbalimbali. Kama mmewahi kupitia baadhi ya ripoti zangu, mtaona maneno haya yametumika mara nyingi katika kukazia maudhui mbalimbali ya hoja za ukaguzi,” alisema CAG.

Spika Ndugai, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa msimamo wake wa kumuita CAG uko palepale na kwamba kumhoji kupitia Kamati ya Bunge ni kuepuka lawama ya kumchukulia hatua za kinidhamu.

Professa Assad analaumiwa kwa kutoa kauli alipokuwa anahojiwa na chombo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Marekani akieleza kuwa kama Bunge halifanyii kazi Ripoti zake ‘huo ni udhaifu wa Bunge’.

Baraza la Habari Kenya laikalia kooni New York Times, laipa saa 24
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 18, 2019