Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameanza kujipigia chapuo kushika nafasi ya juu ya uongozi nchini, akitoa ahadi nono kwa Watanzania.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, ameeleza kupitia Twitter kuwa endapo atapewa nafasi ya kuwa Rais wa nchi, wananchi wake wataishi kwa raha na kustarehe huku wakifanya kazi, kwa lugha ya mtaani ‘watakula bata’.

“Ninaamini nitakuwa Rais bora kwa uwezo wake Mola. Nitauona upinzani kama chachu ya Maendeleo badala ya kuwa na hofu nao. Nitarejesha taswira chanya ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa kwa kulinda Demokrasia na haki za binaadam. Mtachapa kazi, Lakini pia mtakula bata,” ameandika Zitto Kabwe.

 

Katika tweet nyingine, Zitto ameweka picha inayomuonesha akiwa na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na kuwataja baadhi ya vigogo wa upinzani pamoja naye akidai anawataka wafuate sera hiyo.

“Mbobezi Bernard Kamilius Membe Anawasalimu. Hata ikiwa yeye lazima #KaziNabata Au sio jamani? Jamaa yetu T A M Lissu aambiwe pia akiwa yeye #KaziNabata pia maana watu wamechokaaaa. Hata Mzee Edo akiwa yeye tena sisi tunataka #KaziNabata tu,” amendika.

Mwaka 2015, Zitto hakuweza kuwania urais kutokana na kuwa chini ya umri unaokubalika kisheria, lakini chama chake kilimsimamisha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Anna Mghwira ambaye hivi sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi.

Hii inaweza kuwa ni ishara ya nia ya Zitto Kabwe kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Urais mwaka 2020 kupitia ACT-Wazalendo.

Dkt. Bashiru amjibu Membe, atamani kumpigia
WCB wapanga 'kumuwahi' Rich Mavoko apande Wasafi Festival