Wakati baadhi ya wabunge wakipiga kelele kupinga uamuzi wa Serikali kukata kodi kwenye kiinua mgongo chao  kwa mujibu wa Bajeti iliyosomwa Bungeni, Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye hivi sasa anatumikia adhabu ya Bunge, ameendelea kuchochea moto mapato ya wabunge hao kupigwa panga la kodi zaidi.

Akizungumza katika mdahalo wa uchambuzi wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya KPMG juzi usiku, Zitto alipongeza uamuzi wa Serikali kukata kodi kwenye viinua mgogo vya Wabunge, huku akisisitiza kuwa makato hayo yanapaswa kufanyika pia kwenye posho wanazopokea wabunge.

Alisema kuwa Wabunge wanapokea kiasi kikubwa cha Posho kwa shughuli mbalimbali wanazofanya ukiweka kando shilingi 220,000 ya kikao kimoja cha Bunge wanachohudhuria, hivyo wakikatwa kodi kwenye posho hizo mapato ya nchi yataongezeka.

“Nilichokuwa na natarajia ni kuanzisha kodi kwenye posho. Sisi Wabunge tuna posho za aina nyingi na kubwa zaidi ni ile posho ya kikao ya Sh220,000 kwa siku. Hii posho haikatwi kodi na wala siyo fedha za kujikimu (per diem) ambayo unapewa kwa ajili ya chakula na malazi,” alisema.

Alisema kuwa kwa mwaka wabunge hao hupokea posho ya shilingi milioni 40 ambayo ukiizidisha kwa miaka 5 ni zaidi ya shilingi milioni 200, huku kiinua mgogo kikiwa shilingi milioni 172. Hivyo, posho zingeingiza kiasi kikubwa cha mapato ya Serikali zaidi.

Hata hivyo, maoni ya Mbunge huyo wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo hayatapata nafasi ya kuwe sehemu ya Bunge kwani hivi sasa anatumikia kifungo chake cha kutohudhuria vikao vya Bunge hadi Septemba mwaka huu.

Video: 'Mheshimiwa Mpango Usitupeleke Huko, Hatuwezi Kukubali' - Mbunge Kangi Lugola
Kiongozi atakayefanya haya amejitumbulisha