Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtaka Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano.

Afisa Mahusiano wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis amesema kuwa Mkuu wa Upelelezi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam ACP Camilius Wambura amemtaka Zitto kufika kituoni hapo leo majira ya saa tatu asubuhi.

Hata hivyo, Khamis hakueleza sababu zilizotajwa na Jeshi hilo zilizopelekea kutaka kufanya naye mahojiano.

Wito huo wa polisi umekuja siku moja baada ya Zitto kuongoza mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam akizindua operesheni iliyopewa jina la ‘Linda Demokrasia’, huku chama hicho kikipanga kuzunguka nchi nzima kupinga ukandamizwaji wa Demokrasia.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimepinga uamuzi wa Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya kisiasa iliyokuwa imepangwa kufanyika hivi karibuni.

“Sababu zilizotolewa na Jeshi la Polisi kuwa mikutano hiyo inalenga kuchochea wananchi kutotii sheria ni mwendelezo wa visingizio vya Serikali vinavyolenga kuminya uhuru wa wananchi kuikosoa Serikali,” kilisema chama hicho kupitia Taarifa yake iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu.

Young Africans Wamtema Mniger, Wabaki Na Twite
Chadema waambulia Mabomu Kahama, Polisi yapiga marufuku mkutano