Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT – Wazalendo na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amemvaa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akidai kuwa amekuwa akifanya njama za kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli kuonesha kuwa yeye anapanga kumjumu Rais John Magufuli.

Zitto ameeleza kuwa Waziri Kitwanga amekuwa akilalamika na hata alipokaa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na baadhi ya mawaziri kuwa Zitto anafanya mipango ya kumhujumu na kumuondoa katika nafasi ya Uwaziri.

Kiongozi huyo Mkuu wa ACT – Wazalendo amesema kuwa hana nia ya kulumbana na Waziri Kitwanga kwakuwa yeye sio saizi yake na kwamba kiprotokali za uongozi, saizi yake ni Rais Magufuli.

Ameeleza kuwa huwa anamkosoa Rais Magufuli pale anapoona amekosea kwa kuwa yeye ni mzalendo wa kweli na kwamba humueleza moja kwa moja wakati mwingine kwa njia sahihi za kiuongozi lakini pia humpongeza na kuthamini jitihada zake tangu alipoingia madarakani.

Hivi ndivyo alivyoandika kwenye ukurasa wake wa Facebook leo:

Kumekuwa na maneno yanasemwa na mimi kupuuza katika kipindi cha wiki kadhaa; kwamba ninapanga kumhujumu Rais Magufuli katika kazi zake. Maneno haya yanaenezwa na watu wanaotumwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bwana Charles Kitwanga ( nina ushahidi usio na mashaka wa Kitwanga kupanga vijana wa wanaojiita wa UVCCM kufanya mikutano na waandishi wa habari na anawalipa fedha kufanya hivyo. Nataka ifahamike bila chenga kama ifuatavyo:

1) Ninamwunga mkono Rais katika kazi ya kusafisha Nchi. Hii ndio kazi nilikuwa nafanya katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Nitakuwa mtu wa ajabu sana nisipomwunga mkono Rais katika vita dhidi ya Ufisadi. Hata hivyo, kamwe sitasita kuweka wazi pale ninapoona Rais anafanya makosa. Na nimekuwa nikisema wazi wazi na kumkosoa Rais waziwazi. Lakini pia nimekuwa nikimwambia Rais kwa njia nyengine ambazo viongozi huwasiliana ninapoona anafanya sivyo. Kukosoa ni kazi moja muhimu sana na ya kizalendo kuliko lolote ambalo raia anaweza kufanya kwa kiongozi wake. Kukosoa Serikali ni uzalendo maradufu. Pale panapostahili nitapongeza.

2) Namsihi Waziri Kitwanga amalize matatizo yake yeye mwenyewe. Yeye kama mmiliki wa Kampuni ya Infosys yenye mkataba na Serikali katika Wizara anayoongoza sasa anapaswa aone ni namna gani hana mgongano wa maslahi. Waziri Kitwanga asitafute watu wa kuwatupia lawama kwenye mambo yanayomhusu. Mimi binafsi sijawahi kugombana na Charles Kitwanga. Hajawahi kuwa rafiki yangu. Hajawahi kuni excite kama Kiongozi ( kimsingi nashangaa mtu kama yeye kuweza hata kuwa Waziri wa Wizara nyeti kama hiyo) . Zaidi ya yote Waziri Kitwanga sio ‘size yangu’. Kwa protokali za Uongozi, size yangu mimi ni Rais Magufuli, bosi wake. Naanzaje kuhangaika na Kitwanga? Ili iweje? Namsihi asijipandishe chati kwamba mimi nataka kumtoa. Ningetaka kumtoa wala asingejua maana ningeshughulika na aliyemteua. Nasema haya sababu amekaa na Waziri Mkuu na Wabunge kadhaa akilalamika kuwa nataka kumtoa Uwaziri. Asinipe dhambi, Uwaziri atatolewa na aliyemteua kwa madhambi aliyofanya. Asitafute bangusilo!

3) Mimi kwa wiki kadhaa sasa nipo nje ya Nchi ( nchini Marekani katika Chuo Harvard kwa masomo) . Sijui na sihusiki na njama zozote dhidi ya yeyote. Kwanza hizo sio aina ya siasa ninazofanya. Siasa ninazofanya ni Siasa za Maendeleo ya Wananchi na sio Siasa za kuwinda watu.

4) licha ya kuwa Kiongozi wa Chama, Mimi ni Mbunge wa Chama Cha ACT Wazalendo. Kwa hiyo nafuata maelekezo ya chama changu katika kazi zangu. Chama changu katika Mpango Mkakati wake kimeniagiza kufanya Siasa za Maendeleo. Chama changu kinaunga mkono juhudi zote za Rais kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali kwa kupambana na ufisadi. Hata hivyo Chama Cha ACT Wazalendo kinamtaka Rais ajenge mfumo imara wa kitaasisi ili mapambano dhidi ya ufisadi yawe endelevu. Hivyo, porojo za kwamba nataka kumwangusha Rais ni porojo za watu wasionijua binafsi na wasiojua misingi ya ACT Wazalendo

5) Nawasihi Watanzania wote a) kumdharau Waziri Kitwanga na kumtaka ajibu tuhuma zinazomkabili za Kampuni yake binafsi kufanya kazi na Idara katika Wizara anayosimamia na kwamba ajipime kama anatosha kuendelea kumsaidia Rais kazi b) kuendelea kumwunga mkono Rais katika vita dhidi ya ufisadi. Kama nilivyosoma mwaka jana ‘ asiyemwunga mkono Magufuli yupo upande wa mafisadi’ c) kuepuka siasa za porojo zinazoendeshwa na vijana wanaotafuta nafasi za kuteuliwa na d) kutaka umadhubuti wa kila jambo linasomewa ili kuepuka kuonea watu.

 

 

 

Mahakama yafuta Sheria ya ‘matumizi mabaya ya mtandao na vifaa vya mawasiliano’
Mrema kutinga Dar kudai ahadi yake kwa Rais Magufuli