Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameeleza kuwa yapo maeneo muhimu ambayo Rais John Magufuli ameshindwa kutumbua jipu bali majipu hayo yamepapaswa tu.

Akiongea jana katika Mkutano wa Halamshauri ya Taifa ya ACT-Wazalendo, Zitto alisema kuwa chama hicho kinamuunga mkono Rais Magufuli katika juhudi za kupambana na ufisadi na hatua za kutumbua majipu, lakini hakijaridhishwa na kutoguswa kwa kiini cha majipu yenyewe.

Akifafanua kauli yake, Zitto alisema kuwa Sakata la Akauti ya Tegeta Escrow bado linaligharimu Taifa kila mwezi kwa kuwa Kampuni ya IPTL/PAP inaendelea kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 8 kila mwezi kwa ajili ya mitambo ya umeme hata kama hawazalishi.

“Bado huo mtambo upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa Shilingi bilioni 8 wazalishe au wasizalishe umeme. Hivi ndivyo vikundi masilahi katika sekta ya nishati. Bila kuvibomoa, Rais ataonekana anachagua watu katika vita hii,” alisema Zitto.

Kadhalika, Zitto alilitaja sakata la ufisadi katika uuzwaji wa hati fungani za Serikali ambapo alieleza kuwa upande mmoja pekee ndio unaoshughulikiwa baada ya kufikishwa Makamani wakati watoa rushwa wenyewe hawaguswi. Alisema watu waliofikishwa Mahakamani wanashtakiwa kwa rushwa ya dola milioni 6 za Marekani wakiwa kama madalali katika sakata hilo, lakini wahusika zZitto Kabweaidi hawajaguswa huku sakata hilo likipandisha deni la Taifa kwa shilingi Trilioni 1.2.

“Serikali imewafikisha mahakamani madalali wa rushwa lakini waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani. Waliopokea rushwa ambao ni maofisa wa Wizara ya Fedha hawajashtakiwa,” alisema Zitto.

Katika hatua nyingine, alipinga uamuzi wa Serikali kutorusha matangazo ya vikao vya Bunge ‘Live’ na hata kuvizuia vyombo binafsi kufanya hivyo na waandishi wa habari kutoruhusiwa kurekodi chochote bungeni.

Pia, alikosoa uamuzi wa Rais Magufuli kubadilisha matumizi ya fedha zilizopitishwa na Bunge bila idhini ya Bunge ambalo alisema lina jukumu hilo kisheria.

“Rais Magufuli kwani amekuwa waziri wa fedha, waziri wa ujenzi na Rais kwa wakati mmoja?” Alihoji Zitto. “Tunamtaka asiingilie majukumu ya mihimili mingine, wananchi tumnyooshee kidole na kumwambia afuate utaratibu,” aliongeza.

Wiki iliyopita, Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa walitoka nje ya Bunge wakipinga Bunge kutooneshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa lakini pia hata vyombo vya habari binafsi kuzuiwa kufanya hivyo. Pia, walieleza kupinga kile walichodai kuwa Serikali inaingilia majukumu ya Bunge ikiwa ni pamoja na kubadilisha matumizi ya fedha zilizopitishwa Bungeni bila idhini ya Bunge.

 

Aliyebuni jina la ‘Tanzania’ alalamika, aeleza kiasi cha fedha alichopewa na jinsi alivyolibuni
Polisi yawatupa gerezani ombaomba 17, yawashikilia wengine