Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic hatokua sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Sweden kitakachoshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi, kuanzia Juni 14 mwaka huu.

Shirikisho la soka nchini Sweden limethibitisha taarifa hizo, baada ya kuibuka kwa mkanganyiko wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36 kurejea kwenye kikosi cha timu ya taifa cha nchi hiyo, baada ya kutangaza kustaafu miaka miwili iliyopita.

Muda mchache uliopita shirikisho la soka nchini Sweden limetoa taarifa rasmi katika vyombo vya habari, inayoeleza kuhusu Ibrahimovic kuafiki suala la kutokua sehemu ya kikosi, ambacho kitatangazwa majuma kadhaa yajayo.

Shirikisho la soka nchini humo, limetoa taarifa hiyo kupitia kwa mkurugenzi wake wa ufundi Lars Richt, ambaye amethibitisha kufanya mazungumzo na mshambuliaji huyo mpya wa klabu ya LA Galaxy inayoshiriki ligi ya nchini Marekani (MLS).

“Nimezungumza na Zlatan, ameniambia hajabadili msimamo wake wa kuitumikia timu ya taifa, lakini nimemuomba atambue umuhimu wa kutoa nafasi kwa wengine ambao wataitwa kwenye kikosi kwa ajili ya fainali za kombe la dunia, tumefikia muafaka katika hgilo.” Amesema Lars Richt.

Kabla ya kutimkia nchini Marekani, Zlatan kwa kipindi kirefu alikua nje ya uwanja akiuguza majeraha ya mguu, jambo ambalo limemnyima nafasi ya kuwa na utimamu wa mwili, japo kwa sasa anacheza katika ligi ya Marekani.

Mshambuliaji huyo aliweka dhamira ya kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Sweden, na hatua hiyo ilizua mijadala katika mitandao ya kijamii, ambapo wadau wengi wa soka walihoji kwa nini anataka kurejea ili hali ameshatangaza kustaafu soka la kimataifa.

Hadi anatangaza kustaafu soka la kimataifa Zlatan alikua ameshaitumikia Sweden katika michezi 116 na kufunga mabao 62.

Wapigwa marufuku kutumia mtandao wa WhatsApp
RC Makonda atoa msaada kwa familia 600

Comments

comments