Msanii wa muziki wa kizazi kipya Zuhura Othman Soud maarufu Zuchu anatarajia kufanya tamasha kubwa ‘Zuchu Home Coming’ Agosti 21 mwaka huu katika uwanja wa Amani visiwa vya Unguja Zanzibar.

Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo, ambapo amesema kuwa tamasha hilo litashirikisha wasanii wa visiwa hivyo na wengine kutoka Bara.

“Tangu nimeachiwa rasmi na WCB nimekuwa na shauku kubwa ya kutaka kufanya shoo ambayo itaonyesha nia na dhumuni la sanaa ninayoifanya,” amesema Zuch

Zuchu ametaja sababu iliyomfanya kwenda kufanya tamasha hilo Zanzibar ilitokana na tamasha lake la kwanza alilolifanya katika ukumbi wa Mlimani City ‘I am Zuchu’ kuwa kubwa na lililovutia watu wengi.

“Wote tunafahamu kwenye utafutaji unaweza kuishi popote lakini hii hainibagui kwamba mimi ni Mtanzania lakini nimetokea Zanzibar na nimekulia hapa,” amesema Zuchu.

Mkali huyo wa wimbo Sukari, ametaja sababu za kuita tamasha lake ‘Zuchu Home Coming’ kwamba ameita hivyo kwa kuwa anarudi nyumbani lakini pia anaamini mcheza kwao hutunzwa.

“Tutakuwa na wasanii wenzangu kutoka Bara ambao mnawajua, nia na dhumuni kubwa ni kushirikiana na wenzangu naamini hakuna cha mmoja kinachofanikiwa kwa ukubwa cha wengi kinafanikiwa kwa ukubwa,” amesema Zuchu

Aidha msanii huyo amewashukuru wasanii wenzake wa Zanzibar kwa kumpokea vizuri na ushirikiano waliomuonyesha tangu alipowaomba kushiriki katika tamasha lake Agosti 21 kwenye uwanja wa Amani.

Ametaja viingilio katika tamasha hilo kuwa ni pamoja na viti maalum Sh30,000 na ambao watanunua kupitia mtandao wa Zantel itakuwa ni Sh29,000, daraja la pili Sh5000 kwa kawaida ukinunua kwa Zantel utaipata kwa Sh4500 na daraja la kawaida Sh3000 na kwamba tamasha hilo litaanza mchana.

Waziri Ummy: Serikali kuboresha mazingira ya walimu kusikofikika
Waziri Jafo atoa Big Up mradi wa umeme mto Rufiji