Hatimaye Mabingwa wa soka nchini Sudan Al-Merrikh SC wametangaza kuutumia Uwanja wa Pele uliopo mjini Kigali nchini Rwanda, kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Young Africans ya Tanzania.
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza kwa timu hizo umepangwa kupigwa Septemba 16, ambapo Al-Merrikh SC wataanzia nyumbani Pele Kigali, Rwanda, kisha mchezo wa Mkondo wa pili utapigwa Azam Complex, Chamazi Dar es salaam majuma mawili baadae.
Young Africans imethibitisha taarifa za mchezo huo kupigwa Kigali, Rwanda kupitia vyanzop vyake vya habari, ikiandika: Mchezo wetu wa kwanza hatua ya pili #cafcl dhidi ya Al-Merrikh SC utachezwa Uwanja wa Pele Kigali, Rwanda. Tarehe 16.09.2023
Young Africans imesonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuwaondoa ASAS FC ya Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1, michezo yote miwili ikichezwa kwenye Uwanja wa Azam, kufuatia wapinzani wao kutokuwa na Uwanja wa nyumbani wenye viwango kwa sasa.
Msimu uliopita Young Africans ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya mabingwa USM Alger ya Algeria lakini ikakosa taji kwa faida ya mabao ya Ugenini waliyofunga Waarabu hao.
Young Africans ilifungwa mabao 2-1 hapa nyumbani na wakashinda goli 1-0 Ugenini.