Aliyewahi kuwa Kocha wa Viungo wa Simba SC Adel Zrane amesema yupo tayari kurudi kufanya kazi na klabu hiyo endapo Uongozi utamuhitaji.
Zrane aliachana na Simba SC siku chache baada ya klabu hiyo kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya mtoano dhidi ya Jwaneng Galaxy ta Botswana, akiondoka sambamba na aliyekua Kocha Mkuu Didier Gomes Da Rosa.
Zrane amesema hakuna asiyependa kufanya kazi kwenye klabu ya Simba SC, kutokana na mazingira ya klabu hiyo yalivyo, hivyo anatamani kurudi ili aeendelee kuwa sehemu ya Familia ya klabu hiyo.
Katika hatua nyingine Kocha Zrane amethibitisha kuachana na Timu ya Taifa ya Mauritania, baada ya kuondolewa kwa Kocha Mkuu Didier Gomes Da Rosa aliyewahi kufanya naye kazi wakiwa Simba SC.
Gomez alisitishiwa mkataba wake na Shirikisho la Soka la Mauritania mwishoni mwa mwezi Februari, baada ya kushindwa kutimiza wajibu wa kuifikisha mbali timu ya taifa ya nchi hiyo kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika zilizounguruma nchini Cameroon.
“Ni kweli nimeachana na timu ya Taifa Mauritania Kwa sasa sijaongea na timu yoyote japo nimekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya viongozi wa Klabu ya Simba SC.”
“Simba SC ni timu kubwa na ndoto ya Kocha au mchezaji yoyote ni kufanya kazi na timu kubwa hivyo hakuna asiependa kufanya kazi na Simba wakinihitaji niko tayari kurudi Tanzania” amesema Zrane
Zrane amefanya kazi Simba SC na makocha tofauti akianza kwenye Benchi la Ufundi lililokua chini ya Kocha Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck na baadae Didier Gomes Da Rosa kutoka nchini Ufaransa.