Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ya Canada, Profesa John L. Thornton Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 14, 2017.
Mwenyekiti wa Barrick ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited amesema kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imekuwa ikizipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendeleza shughuli zake hapa nchini.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Serikali yake inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalam litakalo fanya mzungumzo na Barrick ili kufikia makubaliano ya kulipa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini kwa maslahi ya pande zote mbili.
Rais Magufuli amesema mbali na mwenyekiti huyo kukubali kulipa fedha zinazodaiwa, pia amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (Smelter) hapa nchini.