Watu 10 wamethibitishwa kufariki Pwani kutokana na Mvua za El-Nino zinazoendelea kunyesha maeneo tofauti nchini Kenya, taarifa ambazo zinakuja ikiwa ni muda mchache tangu kuripotiwa kwa kifo cha Mwanafunzi mmoja mtahiniwa wa KCSE, aalifariki baada ya kupigwa na shoti ya umeme.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Serikali wa eneo la Pwani, Rhodah Nyancha amesema vifo hivyo vimeripotiwa katika kaunti ya Mombasa, Kwale, na Kilifi ambapo mpaka sasa zaidi ya familia 10,000 zimeathiriwa katika eneo la Pwani.
Mapema hii leo, pia viliripotiwa vifo vya Watu watatu mjini Mombasa kutokana Mvua hizo, ambapo mmoja kati ya watu hao alifariki kwa kukanyaga waya wa umeme uliokuwa kwenye maji eneo la Bangladesh – Jomvu kisha wawili walifariki eneo la Tudor, baada ya nyumba yao kuporomoka.
Mamlaka za Serikali nchini humo zinasema mpaka sasa jumla ya watu 3,800 wameathirika na mvua hizo, wakiwemo Maafisa wawili wa mamlaka ya ukusanyaji ushuru – KRA, ambao hawajulikani waliko baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika eneo la Ramisi – Kwale.