Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini kupitia chama cha mapinduzi (CCM), Edward Mwalongo amekutana na kufanya mazungumzo na Wadau wa Kilimo Mjini Njombe juu ya kutumia fursa za masoko ya kilimo ya ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na wadau hao, Mwalongo amesema kuwa lengo la kukutana pamoja ni Kujadili namna bora ya kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo ili kukuza shughuli zao za uzalishaji.
Amesema kuwa Wajasiriamali hao wanatakiwa kutumia fursa zilizopo katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuomba mikopo ili kuongeza thamani ya shughuli zao za Kilimo badala ya kukaa na kulalamika kuwa hawana mitaji.
“Lengo kubwa la kukutana na hawa Wajasiriamali wadogo wadogo wa Jimbo la Njombe Mjini, ni kuwakumbusha namna bora ya kutafuta na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi yetu ikiwemo kupeleka nafaka nchi jirani ya Congo,” amesema Mwalongo.
Aidha, amewataka Wajasiriamali hao kuwa na umoja na mshikamano katika kufanya shughuli zao za Kilimo, ikiwa pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika na kuchakata nafaka ili waingize sokoni kwa haraka.
Kwa Upande wao wadau na Wajasiriamali walioshiriki kikao hicho wamempongeza mbunge huyo kwa kuamua kuwakutanisha pamoja, ili kujadili namna ya kuboresha shughuli zao kwa kutafuta masoko yatakayo kuza thamani ya shughuli zao.
Hata hivyo, wameiomba serikali kupitia mbunge huyo kuwasikiliza na kuwasaidia kwa haraka, pindi wanapofanya michakato ya kuanzisha viwanda vya kusindika bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao ya kilimo kwa lengo la kuisaidia jamii kiuchumi.