Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12 wanaodaiwa kufanya makosa ya udhalilishaji katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Richard Thadei Mchomvu na kudai kuwa kuanzia Novemba 11, 2023 katika vituo vya Polisi Bububu, Madema, Fuoni, Mazizini na Ng’ambo vilivyopo Mkoa wa Mjini Magharibi kuliripotiwa matukio ya udhalilishaji yakieleza watuhumiwa mbalimbali ambao wanadaiwa kufanya makosa ya Ulawiti, Ubakaji pamoja na kuruhusu watoto wa kiume kuingiliana jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kamanda Mchomvu amesema, “baada ya kupokea kwa taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na matukio hayo yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi yalieleza jumla ya wahanga watatu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 17 walifanyiwa ukatili wa kijinsia na watuhumiwa hao.”
Aidha amesema jumla ya kesi tisa zinazohusiana na makosa ya udhalilishaji yamefunguliwa ambapo kati yake majalada manne (04) upelelezi wake umekamilika na yamefikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar na majalada matano upelelezi wake unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo linamshikilia Amour Suleiman Said (41), mkaazi wa Fuoni Zanzibar kwa kosa la kubaka mtoto wa kike ambapo inadaiwa mtuhumiwa huyo katika nyakati tofauti alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 13 ambaye alimchukua tangu akiwa mdogo na kumlea. Baadae inadaiwa mlezi huyo aliingiwa na tamaa ya kingono na kumbaka mtoto huyo jambo ambalo ni kosa.